
Zaidi ya shilingi milioni 21 zimerejeshwa katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026 mkoani Shinyanga kufuatia juhudi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) za kufuatilia matumizi ya fedha za umma, kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na kuchunguza tuhuma mbalimbali za rushwa.
Mafanikio hayo yametangazwa leo Mei 29, 2026 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, ambaye amesema kiasi cha Shilingi 21,897,954/= kimeokolewa baada ya taasisi hiyo kubaini dosari katika matumizi na usimamizi wa fedha za Serikali kwenye maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kessy amesema sehemu ya fedha hizo ni Shilingi 5,540,254/= zilizookolewa kupitia ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Tinde “B” iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambapo ilibainika kuwepo kwa mapungufu katika ulipaji wa baadhi ya kodi na ushuru wa Serikali.
Amefafanua kuwa katika mradi huo, kiasi cha Shilingi 5,316,304/= kilitakiwa kulipwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama kodi ya zuio maarufu kama withholding tax, huku Shilingi 223,950/= zikiwa ni ushuru wa huduma ambao haukuwa umelipwa kwa wakati unaotakiwa kisheria.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, hatua hizo zinaonyesha namna ufuatiliaji wa karibu wa matumizi ya fedha za umma unavyoweza kusaidia kudhibiti ubadhirifu na kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.
Mbali na kurejesha fedha hizo, taasisi hiyo pia imeendelea kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi na wadau mbalimbali ili kuongeza uwajibikaji, uwazi na ushirikiano katika kusimamia rasilimali za umma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) katika Wilaya ya Kishapu, hatua iliyosaidia baadhi ya AMCOS zilizokuwa zikidaiwa na makampuni ya ununuzi wa pamba kurejesha madeni yenye thamani ya Shilingi 9,322,000/=.
Aidha, Kessy ametoa wito kwa taasisi za umma kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na sheria zilizowekwa, huku akiwaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU katika vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu ili kulinda fedha za umma na kuharakisha maendeleo ya taifa.


Social Plugin