Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAZINDUA PROGRAMU YA KUIMARISHA UONGOZI SHULE ZA SEKONDARI NCHINI


Na Mwandishi wetu, Mwanza.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknologia pamoja Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) imezindua rasmi programu kubwa ya mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa elimu kwa shule za Sekondari nchini.

Programu hiyo ambayo inatekelezwa na Wakala wa Maendeleo ya uongozi wa Elimu Tanzania (ADEM) kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Maendeleo la Ubelgiji (VVOB) inatarajia kutekelezwa katika mikoa yote 31 Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo iliyofanyika Jijini Mwanza jana, Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Maulid Maulid alisema kuwa zaidi ya viongozi wa Elimu 16,000 wanatarajiwa kufikiwa na programu hiyo.

Alisema kuwa kati ya viongozi hao, walimu wakuu wa shule za Sekondari pamoja na wasaidizi wao watakaofikiwa na Programu hiyo ni 12,000 huku waratibu elimu watakaofikiwa wakiwa ni 4,000 nchi nzima.

Mtendaji mkuu huyo alisema kuwa programu hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika maeneo ya uongozi wa kimkakati na misingi ya Utawala Bora Shuleni, Maadili ya Ualimu na Itifaki za Uongozi wa Elimu.

Maeneo mengine aliyotaja Dkt. Maulid ni Ujumuishaji wa jamii katika shughuli za Shule, Uongozi unaohimiza Usimamizi bora wa ufundishaji na ujifunzaji, uthibiti ubora wa ndani, usimamizi wa Mfumo wa MEWAKA Shuleni pamoja na Matumizi ya TEHAMA katika Uongozi.

“ Mwaka 2015 ndio wakati wa mwisho ADEM iliweza kuandaa mafunzo makubwa ya uongozi kwa wakuu wa shule za sekondari nchini kwa kiwango cha kitaifa, pengo hilo la zaidi ya miaka kumi lilikuwa na athari kubwa”….

“ wakuu wengi wa shule waliopata mafunzo wakati huo tayari wamestaafu au wamepanda vyeo, na kizazi kipya cha wakuu wa shule walioingia madarakani baada ya 2015 hawakupata mafunzo rasmi ya uongozi kutoka kwa taasisi hii ya Serikali”

Kwa upande wake Meneja wa Programu hiyo nchini kutoka Shirika la kimataifa la Maendeleo la Ubelgiji (VVOB) Sarish Haribae alisema kuwa program hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2025 hadi 2030.

Haribae alibainisha kuwa kwa miaka ya hivi karibuni dunia ya elimu imekuwa ikibadilika badilika kwa kasi kubwa, mabadiliko ambayo yanahitaji kuwa na viongozi wa shule wenye uwezo kuleta matokeo chanya kwa walimu, wanafunzi na shule kwa ujumla.

Akizindua Programu hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknologia Prof. Carolyne Nombo alisema kuwa ujio wa programu hiyo itasaidia kuboresha mfumo wa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA).

Prof. Nombo alisema kuwa sekta ya elimu haiwezi kuwa na mabadiliko endapo watendaji wake hawataweza kuhimarika katika namna bora ya kuendesha kile wanachokisimamia.

 “ Miaka mitatu iliyopita serikali imefanya maboresho makubwa ya sera mpya ya elimu, mabadiliko hayo ya sera yanalazimisha kila mtendaji katika sekta ya elimu aweze kubadilisha namna ya utendajikazi na utolewaji wa elimu nchini,” alisema Prof Nombo.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com