Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFANYA MAWASILIANO NA MAREKANI KUHUSU TUHUMA ZA UBAGUZI WA KIDINI

 

Serikali imesema imeanza kufanya mawasiliano rasmi kuhusu tuhuma zilizotolewa na Marekani dhidi ya Tanzania, huku ikisisitiza kufuata misingi ya kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, aliyasema hayo bungeni Dodoma kufuatia hatua ya Ubalozi wa Marekani nchini kueleza kuwa baadhi ya wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la nchi hiyo wamependekeza kupitia upya uhusiano kati ya mataifa haya mawili sambamba na madai ya kuwepo kwa ubaguzi wa kidini nchini Tanzania.

Balozi Kombo alibainisha kuwa hadi sasa serikali haijapokea taarifa yoyote rasmi ya maandishi kuhusu madai hayo yaliyozungumzwa, bali imeona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya ubalozi huo. 

Alifafanua kuwa utaratibu huo uliotumiwa na ubalozi ni kinyume na miongozo ya kidiplomasia kwani walitakiwa kuwasilisha malalamiko yao kwa mujibu wa taratibu na Mwongozo wa Vienna unaosimamia mahusiano ya kimataifa.

Waziri aliongeza kuwa serikali ina utaratibu madhubuti na maalumu wa kushughulikia hoja zote zinazotolewa dhidi ya nchi kupitia njia sahihi za kidiplomasia kama inavyofanyika kwenye hoja za mabunge mengine duniani. 

Ili kupata muafaka na ufafanuzi wa kina, mawasiliano ya moja kwa moja tayari yameanza kupitia Balozi wa Tanzania nchini Marekani aliyepo Washington DC ambaye anafuatilia suala hilo kwa ukaribu.

Wakati huohuo, wabunge wamepinga vikali madai hayo wakisema hayana ukweli wowote ndani ya jamii ya Kitanzania. Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, alieleza bungeni kuwa katika umri wake wote wa miaka 37 hapa duniani, hajawahi kushuhudia, kuhisi, wala kunusa chembechembe zozote za ubaguzi wa kidini au mgawanyiko wa kitaifa nchini Tanzania, akisisitiza kuwa nchi imeendelea kubaki salama na yenye mshikamano. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com