Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIMAMO WA VIONGOZI WA DINI: TUHUMA ZA MAREKANI JUU YA UDINI TANZANIA NI UZUSHI MTUPU

 

Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania imesimama kidete na kutangaza kuwa nchi ina amani ya kutosha na uhuru kamili wa kuabudu, mambo ambayo yamejengwa katika misingi ya kuheshimiana kidini na kuifanya kuwa miongoni mwa mataifa yenye utulivu mkubwa zaidi barani Afrika. 

Katibu wa jumuiya hiyo, Mchungaji Dk. Israel Maasa, alitoa kauli hiyo wakati akisoma tamko rasmi kufuatia taarifa zilizosambazwa na Ubalozi wa Marekani nchini zikidai kuwa baadhi ya wabunge wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Marekani wamependekeza kupitia upya uhusiano wao na Tanzania kutokana na shutuma za kuwepo kwa ubaguzi wa kidini. 

Dk. Maasa alifafanua kuwa tangu kupatikana kwa uhuru, Watanzania wa dini zote wamekuwa wakiishi kwa mshikamano wa kijamii, wakioana, wakifanya biashara kwa pamoja, na kujenga urafiki wa damu bila ubaguzi wowote.

Katika kuonyesha jitihada za ndani za kuimarisha utulivu, viongozi hao walibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha nia thabiti ya kushughulikia mapungufu yote yaliyotokea mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kuunda tume maalumu ya uchunguzi na nyingine ya kijinai ili kuhakikisha uwajibikaji na maridhiano vinachukua nafasi yake. 

Dk. Maasa alitoa rai kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuunga mkono mazungumzo ya kidiplomasia yanayojenga badala ya kutoa kauli zinazoweza kuleta migawanyiko katika jamii yenye misingi imara ya imani mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Alhad Mussa Salum, alilaani vikali kauli zilizotolewa na maseneta wawili wa Marekani kuhusu hali ya uhuru wa dini nchini akizitaja kuwa zimejaa uzushi na hazina ukweli wowote wa kiuhalisia. 

Salum alisema madai hayo yaliyolenga kuonyesha kuwa Tanzania si salama na ina ubaguzi yameumiza hisia za Watanzania kwa sababu yanapotosha hali halisi ya maisha ya kila siku. 

Alisisitiza kuwa uwepo wa viongozi wa dini mbalimbali kwa pamoja katika kutoa tamko hilo ni kielelezo tosha kuwa Wakristo na Waislamu nchini humo ni ndugu wa damu na hakuna taifa lolote la nje linaloweza kuwagombanisha kwa kutumia karata ya udini kwani mbinu hizo zimepitwa na wakati.

Viongozi hao walihitimisha kwa kuipongeza serikali kwa namna ya kipekee ilivyosimamia na kushughulikia changamoto zilizojitokeza, hatua ambazo zimesaidia kuongeza mshikamano kitaifa. Salum aliongeza kuwa matukio yote yaliyojitokeza huko nyuma, ikiwemo yale ya mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana, hayajaiyumbisha Tanzania bali yameendelea kuijenga, kuinoa, na kuifanya kuwa taifa imara zaidi ambalo haliwezi kubomoka kirahisi kwa propaganda za nje.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com