Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERA, USIMAMIZI MZURI NA DHAMIRA NJEMA YA RAIS SAMIA YAONGEZA IDADI YA WAGENI NCHINI



Na mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Mambo ya ndani Mhe. Patrobas Katambi amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026 jumla ya wageni 2,005,209 waliingia Nchini ikilinganishwa na 1,839,342 walioingia katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25, suala ambalo limechagizwa na jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya kuvutia wageni katika sekta za utalii, uwekezaji na huduma za kijamii Nchini.

Waziri Katambi ameyasema hayo leo Mei 25, 2026 wakati wa hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2026/27, Bungeni Mjini Dodoma, akisema katika kipindi hicho pia jumla ya Watanzania 476,190 walitoka Nchinu na 443,561 walirejea Nchini, ikilinganishwa na watanzania 400,434 waliotoka na 376,011 waliorejea katika kipindi kama hicho kwa mwaja 2024/25.

"Aidha katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, jumla ya Pasipoti 78,583 zilitolewa kwa Watanzania ikilinganishwa na Pasipoti 114,448 zilizotolewa kwa kipindi kama hiki kwa mwaka 2024/25. Aidha hati za safari za dharura 226,400 zilitolewa ikilinganishwa na hati 204,387 zilizotolewa kwa mwaka 2024/25." Amekaririwa Waziri Katambi.

Waziri Katambi katika hatua nyingine amesema ili kukabiliana na uhamiaji haramu hususani katika Mikoa ya mipakani, Wizara yake kupitia Idara ya uhamiaji imeanzisha kanda maalum za uhamiaji katika mikoa ya Kagera na Kigoma, akisema Idara hiyo pia itaendelea kufanya misako, doria na kuanzisha Kanda nyingine katika maeneo ya kimkakati na yenye muingiliano mkubwa wa wageni ili kuhakikisha wahamiaji haramu wanadhibitiwa ipasavyo.

Waziri Katambi pia ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kushirikiana na idara ya uhamiaji katika kuwafichua wageni wanaoishi katika maeneo yao kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi, akisema kufanya hivyo kutaifanya Tanzania kuendelea kuwa salama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com