Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT)
Askofu Israel Maasa, amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa duniani kwa kudumisha amani, mshikamano na uhuru wa kuabudu kwa wananchi wa dini zote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Askofu Maasa amesema kwa zaidi ya nusu karne, Watanzania wameishi kwa upendo, kuheshimiana na kushirikiana bila kujali tofauti zao za kiimani, jambo ambalo limeifanya Tanzania kuwa taifa lenye utulivu na mshikamano wa kitaifa barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, amesema JMAT imesikitishwa na taarifa zilizotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania zinazodai kuwepo kwa ubaguzi wa kidini nchini, akieleza kuwa madai hayo hayana uhalisia wa mazingira halisi ya Tanzania.
Amesema taarifa hizo, ambazo pia zinadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya wabunge pamoja na Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Marekani, zimewasikitisha wananchi wengi kwani zinatoa taswira isiyo sahihi kuhusu hali ya uhuru wa dini nchini.
“Watanzania wameendelea kuishi kwa amani na mshikamano mkubwa kwa miaka mingi bila migogoro ya kidini. Hakuna anayebaguliwa kutokana na imani yake,” amesema Askofu Maasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JMAT, Alihadi Mussa Salum, amesema hakuna kundi lolote nchini linalonyimwa haki ya kuabudu au kufanyiwa vitendo vya ukandamizaji kwa misingi ya dini, dhehebu au imani.
Amesema Tanzania imejengwa katika msingi wa umoja wa kitaifa, amani na mshikamano, hivyo watu wanaoeneza taarifa zinazoweza kuigawa jamii au kuipa nchi taswira ya ubaguzi wanapaswa kuacha kufanya hivyo.
Aidha, JMAT imeitaka Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya tathmini ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani, ikieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kulinda mshikamano wa kitaifa dhidi ya taarifa zinazoweza kuchochea migawanyiko ya kidini.



Social Plugin