Na mwandishi wetu , Dodoma
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imewaondoa hofu wafugaji wa samaki kwa vizimba nchini kuhusu upatikanaji wa chakula cha samaki na vifaa vya ufugaji, ikisema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu na yenye tija.
Hayo yameelezwa leo Mei 26,2026 bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Dkt Bashiru Ali wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya(CCM)
Katika swali lake Mbunge huyo amehoji kuhusu changamoto ya upatikanaji wa chakula cha samaki kwa ufugaji wa vizimba na lini Serikali itawapatia boti za kisasa wafugaji wa Wilaya ya Bunda.
Akijibu,Dkt Bashiru amesema Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa chakula cha samaki, huku akieleza kuwa tatizo hilo linachangiwa na kukua kwa kasi kwa shughuli za ufugaji wa samaki kwa vizimba nchini.
Amesema ufugaji wa vizimba ni sekta mpya inayopanuka kwa kasi na hivyo kuongeza mahitaji ya chakula cha samaki, hali ambayo imekuwa ikisababisha changamoto ya upatikanaji wake kwa wakati.
Hata hivyo, amesema hali hiyo inaanza kuimarika baada ya kuongezeka kwa viwanda vya uzalishaji wa chakula cha samaki, ikiwemo kiwanda kilichopo Dar es Salaam pamoja na vingine vilivyoanzishwa Mwanza na maeneo mengine na wawekezaji binafsi.
“Kadri wazalishaji wa chakula cha samaki wanavyoongezeka, bei nazo zinaendelea kushuka na kufanya shughuli za ufugaji kuwa nafuu zaidi,” amesema Waziri huyo.
Ameeleza kuwa chakula cha samaki kinachukua zaidi ya asilimia 70 ya gharama zote za ufugaji wa samaki kwa vizimba, hivyo Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uzalishaji na upatikanaji wake ili kupunguza gharama kwa wafugaji.
Kuhusu mahitaji ya boti za kisasa kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa vizimba wilayani Bunda, Waziri amesema Serikali imeunda tume maalumu ya kupitia na kuboresha mfumo wa utoaji wa boti hizo ili kuhakikisha zinakidhi viwango na mahitaji halisi ya wafugaji.


Social Plugin