Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU: RAIS SAMIA AWEZESHA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII KUWA HIMILIVU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu akitoa ufafanuzi kwa Waheshimiwa Wabunge, wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2026/2027 katika Bunge la 13, Mkutano wa Tatu, kikao cha Tisa leo Aprili 15, 2026 Jijini Dodoma.

************

Na: OWM (KAM) – Bungeni, Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini kwa lengo la kuhakikisha ustawi wa wananchi, pamoja na kuhakikisha utoaji wa pensheni kwa wakati.

Pongezi hizo zimetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu, leo Aprili 15, 2026 wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2026/2027.

Aidha, Mhe. Sangu amesema thamani ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeendelea kuongezeka ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) thamani yake imeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 4.36 hadi Shilingi Trilioni 10.3. Mfuko wa PSSSF thamani yake iliongezeka kutoka Shilingi Trilioni 5.74 hadi Shilingi Trilioni 12.96.

Waziri Sangu amefafanua kuwa deni la Serikali katika mfuko wa PSSSF ilikuwa Trilioni 4.46, mwaka 2022/2023 Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa hati fungani ya shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kuulipa mfuko wa PSSSF deni lililodumu kwa muda mrefu la shilingi trilioni 4.6 la michango kabla ya 1999. Pia, Serikali imeendelea kulipa Trilioni 2.09 ambayo imesaidia thamani ya Serikali kulipa mfuko huo wa PSSSF kufikia asilimia 95.

Vilevile, Mhe. Sangu amesema kuwa kutokana na mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa himilivu imepelekea kwa sasa watumishi wa umma wanaostafu wanalipwa mafao yao ndani ya siku ishirini na tano huku kiwango cha kima cha chini cha pesheni kuongezeka toka shilingi 100,000 hadi kufikia shilingi 250,000 kwa wastaafu.

Kadhalika, Waziri Sangu amesema Mifuko ya hifadhi ya jamii imeendelea kuwekeza katika miradi yenye tija kwa lengo la kuongeza thamani ya michango ya wanachama na kukuza uchumi pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi.

Akihitimisha mchango wake, Mheshimiwa Sangu aliwahakikishia wabunge kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano itaendelea kusimamia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ufanisi, ili kuleta manufaa kwa Watanzania katika sekta zote za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Mussa Azan Zungu, amewapongeza wabunge kwa kupitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kusisitiza umuhimu wa wizara na taasisi husika kusimamia utekelezaji wake ili kuchochea maendeleo ya wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com