
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi imeendelea kujidhihirisha kuwa kitovu kipya cha mvuto wa utalii wa ndani, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Hamis, kuvutiwa na upekee wa vivutio vilivyopo hifadhini humo.
Katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, Mhe. Hamida alijionea kwa karibu utajiri wa rasilimali za wanyamapori, akieleza kuwa uzoefu alioupata ni ishara tosha kwamba Tanzania ina hazina kubwa ambayo bado haijatumika kikamilifu kuwavutia Watanzania wenyewe.
“Nilichokiona hapa ni tofauti kabisa; ndani ya muda mfupi tu tayari tulikuwa tumeshuhudia simba. Hii inaonesha namna ambavyo vivutio vyetu vina nguvu ya kipekee,” alisema kwa msisitizo.
Akiangazia nafasi ya Zanzibar katika ramani ya utalii, Mhe. Hamida alisema visiwa hivyo vinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza utalii wa Bara ikiwa juhudi za makusudi zitawekwa katika kuwaunganisha watalii hao.
Alieleza kuwa kuna umuhimu wa kubadili mtazamo wa utalii kwa kuondoa dhana kwamba ni shughuli ya wageni pekee, badala yake kuwa sehemu ya maisha ya Watanzania.
“Tunapaswa kuufanya utalii kuwa sehemu ya utamaduni wetu. Tukianza sisi, hata wageni wataona thamani halisi ya nchi yetu,” aliongeza.
Katika mtazamo wa maendeleo ya sekta hiyo, alibainisha kuwa uwepo wa miundombinu ya kisasa kama reli ya SGR na huduma za anga unatoa nafasi kubwa kwa ukuaji wa utalii wa ndani kwa kasi zaidi.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Masesa, alisema hifadhi hiyo imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani, hasa kutoka Zanzibar.
Alisema ongezeko hilo linaakisi mafanikio ya juhudi za kuitangaza Tanzania kupitia kampeni ya Royal Tour pamoja na uelewa unaoongezeka kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vya ndani.
Masesa aliongeza kuwa Mikumi inaendelea kuwa lango muhimu la utalii, akiwahimiza Watanzania kutumia fursa hiyo kujionea uzuri wa nchi yao badala ya kusubiri simulizi kutoka kwa wengine.

















Social Plugin