Aprili 13,2026, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kombo, alikutana na kuzungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini Mauritius katika Chuo Kikuu cha Middlesex na kuwashauri wanafunzi hao kuhusu maisha yao ya masomo pamoja na wajibu wao wa kuiwakilisha Tanzania wakiwa ugenini.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Kombo, ambaye aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Mauritius mwenye makazi yake Harare, Zimbabwe, aliwahimiza wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri wa nchi yao na kuzingatia maadili mema ya Kitanzania, nidhamu, na mwenendo unaoendana na heshima ya taifa.
Alisisitiza umuhimu wa kuitangaza Tanzania vyema popote walipo na kuepuka kuwaangusha wazazi wao waliowezesha safari yao ya elimu na kueleza kuwa juhudi zao zinapaswa kuonekana si tu kitaaluma bali pia kitabia.
“Ninyi ni mabalozi wa taifa lenu, hivyo muiwakilishe vyema nchi yenu na msiwaangushe wazazi wenu.
Nimezungumza na Mkuu wa Chuo, amenihakikishia kuwa wanafunzi wa Tanzania mnafanya vizuri na hamna changamoto za kinidhamu,” alisisitiza Balozi Kombo.
Aliwahamasisha wanafunzi hao kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya ili kupata taarifa sahihi na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali kama za ajira, ufadhili wa masomo na mafunzo yatakayowasaidia kukuza taaluma zao na kujijengea uwezo wa kiuchumi.
Waziri Kombo pia alitahadharisha dhidi ya majaribu yanayoweza kuwapotosha vijana wakiwa nje ya nchi na kuwasihi kuepuka matumizi ya dawa za kulevya, akieleza kuwa baadhi ya vijana hujikuta wakiharibu mustakabali wao kutokana na tamaa ya kujaribu mambo yasiyofaa.
“Msijaribu kila kitu, kuweni na maadili mema na epukeni matumizi ya dawa za kulevya ili muwe vijana bora na viongozi wa kesho,” alionya.
Ziara hiyo ilifanyika sambamba na ushiriki wa Waziri Kombo katika Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi uliofanyika Aprili 10 hadi 12 jijini Port Louis, uliowakutanisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi 30 zinazozunguka Bahari ya Hindi kujadili fursa, changamoto na maendeleo ya ukanda huo.


















Social Plugin