Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATANZANIA WATAKIWA KUENZI MISINGI YA MUUNGANO


Katika kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema mafanikio ya Muungano huo yanatokana zaidi na mshikamano wa watu kuliko mifumo ya kiserikali.

Ameeleza kuwa Muungano wa Tanzania ni wa kipekee barani Afrika kwa kudumu kwa zaidi ya miongo sita, tofauti na miungano mingine iliyoshindwa kuhimili misukosuko ya kisiasa na kijamii ndani ya muda mfupi.

“Wetu ni muungano wa watu zaidi ya serikali. Ni miaka 62 sasa, na huu ndio Muungano pekee wa mataifa mawili huru barani Afrika uliofanikiwa kudumu kwa muda mrefu kiasi hiki,” amesema Kafulila.

Alifafanua kuwa mifano ya miungano iliyovunjika ni pamoja na ule wa Ethiopia na Eritrea uliodumu kati ya mwaka 1952 hadi 1962, pamoja na muungano wa Ghana, Guinea na Mali (1958–1963), na ule wa Senegambia (1982–1989), ambayo yote ilidumu kwa muda mfupi kabla ya kuvunjika.

Kwa mujibu wa Kafulila, siri ya uimara wa Muungano wa Tanzania ipo katika misingi yake ya kijamii na kitamaduni, ikiwemo udugu wa kihistoria, matumizi ya lugha ya Kiswahili na mshikamano wa watu wake.

Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kuthamini na kuuenzi Muungano huo kwa kuzingatia misingi iliyoasisiwa na viongozi wa awali, akiwemo Julius Nyerere na Abeid Karume.

Kauli hiyo imekuja wakati Watanzania wakiendelea kuadhimisha miaka 62 ya Muungano, wakitafakari mafanikio, changamoto na mustakabali wa ushirikiano huo wa kihistoria.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com