Na mwandishi wetu, Dar
Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi wa ghasia wakati na baada ya uchaguzi, Ibrahim Juma, ameeleza kuwepo kwa tabia hatari inayoendelea kujitokeza nchini ya baadhi ya watu kutovumilia maoni tofauti, hali inayowapelekea kuyakandamiza kwa matusi na kudai kusikilizwa kwa upande wao pekee.
Profesa Juma amesema hali hiyo imejidhihirisha wazi hata baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya tume hiyo, ambapo baadhi ya wajumbe wamepokea jumbe zaidi ya 300 za matusi kupitia simu zao, kutoka kwa watu waliopinga maudhui ya ripoti hiyo kwa lengo la kuzuia maoni yaliyotolewa kwa misingi ya kitaaluma kufikia jamii.
Ameeleza kuwa kitendo hicho ni ishara ya changamoto ya uvumilivu wa kisiasa na kijamii, ambapo baadhi ya wananchi wanashindwa kukubali mitazamo tofauti inayotokana na utafiti na uchambuzi wa kitaalamu uliofanywa kwa kutumia mbinu za kusikiliza wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Jumanne Aprili 28, 2026, Profesa Juma alisema matusi hayo yanadhihirisha wazi kuna watu ambao hawataki kuona maoni yaliyotolewa kupitia njia ya kisayansi na uchambuzi yakinifu yakifikia umma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa jamii kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kusikilizana na kuheshimu maoni tofauti, akieleza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea mjadala huru na wa staha badala ya matusi na vitisho.
Kwa mujibu wake, ni muhimu kwa wananchi kuelewa kuwa tofauti za maoni ni sehemu ya demokrasia na hazipaswi kuwa chanzo cha uhasama au matusi, bali kujenga msingi wa majadiliano yenye tija kwa taifa.

Social Plugin