Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI DODOMA KUNUFAIKA NA AWAMU YA PILI YA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambapo awamu ya pili ya kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika mkoani Dodoma kuanzia Mei 1 hadi 15, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 29, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan makundi yenye uhitaji kama wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha haki inapatikana kwa urahisi kupitia huduma za msaada wa kisheria zinazotolewa bure kwa wananchi.

Kwa mujibu wa takwimu za utekelezaji wa awamu ya kwanza mwaka 2023, Mkoa wa Dodoma ulifanikiwa kuwafikia wananchi 86,947 waliopatiwa huduma za msaada wa kisheria, ambapo kati yao wanaume walikuwa 42,298 na wanawake 44,649.

Aidha, jumla ya migogoro 818 ilipokelewa, huku migogoro 452 ikitatuliwa na mingine 366 ikiendelea kufanyiwa kazi.

Senyamule amesema mafanikio hayo yanaonesha uhitaji mkubwa wa huduma za msaada wa kisheria, hali iliyosababisha Serikali kuendelea na awamu ya pili ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata haki zao kwa wakati na kwa urahisi.

Katika kampeni hiyo, huduma mbalimbali zitatolewa bila malipo ikiwa ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu ya sheria kwa jamii, uandaaji wa nyaraka za kisheria, uwakilishi mahakamani na kwenye mabaraza, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na huduma za usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Ameeleza kuwa eimu kwa umma itatolewa katika ngazi zote kuanzia wilaya hadi vijiji na mitaa, sambamba na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama masoko, vituo vya mabasi, taasisi za elimu na mikusanyiko ya kijamii.

Pia Vituo vya utoaji huduma vitaanzishwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na kampeni hiyo, akisisitiza kuwa haki ni msingi wa maendeleo na kila mwananchi anapaswa kupata ulinzi wa haki zake.

Pamoja na mambo mengine Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ikiwa inaakisi dira ya taifa ya kujenga jamii yenye usawa na ustawi kwa wote ifikapo mwaka 2050.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com