Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUNAHITAJI MSAMAHA KUPONYA TOFAUTI ZETU ZA KISIASA NA KIJAMII- ASKOFU HOTAY



Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Arusha na Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro Stanley Hotay amesema Taifa la Tanzania linahitaji msamaha ili kuponya majeraha yanayotokana na tofauti na migawanyo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, akisisitiza wito wa kila mmoja kusamehe kama maandiko Matakatifu yanavyotaka.

Askofu Hotay ametoa kauli hiyo Aprili 03, 2026 wakati akihubiri katika ibada ya Ijumaa kuu ya Umoja wa Makanisa Mkoa wa Arusha, ibada iliyofanyika katika Viwanja vya Kanisa la Jimbo kuu Katoliki St. Theresa, Arusha, akisema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa fursa kwa Watanzania kuchagua lililo jema kwa kuacha kiburi na ujeuri na badala yake wakumbatie msamaha kama msingi wa umoja wa Kitaifa.

"Katika siku hii ya Ijumaa Kuu, siku muhimu sana, chagua lililo jema. Tanzania kama sehemu ya kuishi tunahitaji msamaha kila siku, kusamehewa ni kufunguliwa na si fedheha wala aibu. Kusamehewa kutokana na majeraha ya kisiasa, kibiashara, kijamii na migawanyiko na majeraha tuliyoyapata kutokana na kutofautiana kwetu, sisi Watanzania tunahitaji msahama na Biblia inasema kwa ukali kuwa mtu hupungiwa neema ya Mungu na shina la uchungu huzaliwa ndani yake kutokana na kutosamehe." Amesema Askofu Hotay.

Askofu Hotay amesisitiza kuwa msalaba wa Yesu si tu mahali pa kuteswa kwa Kristo bali ndipo mahali nguvu ya kusamehe inapopatikana, akiwataka Watanzania kufahamu kuwa Ijumaa kuu imebeba ujumbe muhimu kwa Watanzania, ikiangazia familia na Taifa kwa ujumla, akiwataka kuelewa thamani ya kweli ya gharama iliyolipwa msalabani, akisema msamaha si aibu wala fedheha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com