Na Dotto Kwilasa, DODOMA
ASKOFU wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani, amewahimiza Watanzania kuitumia siku ya Ijumaa Kuu kama fursa ya kusameheana, kuacha ubinafsi na kusahau changamoto zilizopita, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu jijini Dodoma, Askofu Chilongani amesema siku hiyo takatifu, inayokumbusha mateso na kifo cha Yesu Kristo, inapaswa kuwa chachu ya kuanzisha upendo mpya miongoni mwa Watanzania.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki, taifa linaendelea kushuhudia dhamira ya dhati ya Serikali ya kudumisha amani, utulivu na kuimarisha maridhiano.
Kiongozi huyo wa kiroho amebainisha kuwa viongozi wa dini na serikali wana jukumu la pamoja la kuhamasisha mshikamano, kuondoa chuki na kujenga mazingira ya maelewano.
Amesisitiza kuwa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeweka msingi imara wa kuendeleza ajenda ya maridhiano na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
“Ni muhimu kwa viongozi wa serikali kuendelea kutumia nafasi zao kuhimiza misamaha, kuondoa vikwazo na kujenga upendo miongoni mwa wananchi,haya ni mambo ambayo tayari yanaonekana chini ya uongozi wa sasa,” amesema Askofu Chilongani.
Ameongeza kuwa ili kujenga taifa lenye afya na maendeleo endelevu, ni lazima wananchi waepuke ubinafsi na chuki, badala yake wajenge utamaduni wa kusameheana, kuheshimiana na kushirikiana.
Amesisitiza kuwa msamaha si jukumu la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania, akieleza kuwa msamaha ni tendo la kiimani linalochochea amani, utulivu na maendeleo ya taifa.

Social Plugin