Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TPHPA YANG'ARISHA MEI MOSI NJOMBE, MAKAMPUNI 16 YAPATA SOKO LA PARACHICHI CHINA


Mwandishi wetu,Arusha

Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeng'arisha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi ambayo yatafanyika mkoani Njombe, kwa kuwezesha kampuni 16 za kilimo cha parachichi na viazi, kupata masoko nchini China, huku pia ikitarajiwa kuanza ujenzi wa Maabara ya kupima ubora wa mazao hayo mkoani Njombe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei mosi mwaka huu, mkoani Njombe na tayari, Mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka ametangaza mkoa huo kujiandaa vyema kwa maadhimisho hayo.

TPHPA inatarajia  katika sehemu ya maadhimisho hayo, kuwekwa  jiwe la msingi Jengo la Maabara  ya mazao ya  kimkakati  Mei Mosi, hatua ambayo inatarajiwa kuwanufaisha maelfu ya  wakulima wa mazao ya parachichi, Viazi  mviringo na mengine, kupata hati za ubora wa mazao yao kwa ajili ya masoko ya kimataifa   mkoani Njombe badala ya kuyasafirisha kwenda maeneo mengine ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa  Joseph Ndunguru   akizungumza na Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma pamoja na wanachama wa JOWUTA,  Leo April 20,2026 amesema Mamlaka hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wakulima na wafanyakazi nchini wananufaika na kilimo cha mazao ya kimkakati.

Profesa Ndunguru kwa sasa wamewezesha usajili wa makampuni 16 ya mazao ya kimkakati kupata masoko nchini China lakini pia mkakati wa kusaidia wakulima wengine unaendelea katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

"Tunawasaidia wakulima kuweza kuuza bidhaa zao nje ya nchi, kwa kuzipima na kuziondolea  mabaki ya viatilifu vyovyote  ambavyo vinawezakuwa kubaki katika mazao yao",amesema.

Amesema katika kuendeleza kazi hiyo, Mamlaka hiyo, itaanza karibuni ujenzi wa maabara katika mji wa Makambako ambayo itasaidia sana hata wakulima wadogo wadogo kupata masoko ya uhakika nje ya nchi.

Akizungumzia  maadhimisho ya Mei Mosi, Ndunguru amesema Mamlaka hiyo kama ilivyo kawaida itashiriki ipasavyo katika ngazi mbali mbali hadi taifa na itashirikiana na JOWUTA kuhakikisha inatimiza wajibu wake, ikiwepo kuhabarisha umma kazi nzuri ambazo zinafanywa na Serikali.

Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma akizungumza na Mkurugenzi huyo, alimpongeza kwa kazi nzuri ambayo TPHPA wamekuwa wakifanya  ambayo sasa inahakikisha usalama walaji wa mazao mbali mbali ambayo yanazalishwa hapa nchini na wakulima 

"TPHPA inafanyakazi kubwa na sisi  wanahabari tunawapongeza kwa sababu mmeweza kudhibiti kuingia nchini viatilifu visivyo na ubora, mmekuwa mkiwasaidia wakulima  kuzingatia afya zao na walaji katika matumizi ya viatilifu, kuwasaidia kupata masoko ya uhakika nje ya nchi  lakini pia mmekuwa mkisaidia tafiti nyingi za masuala ya afya ya mimea na vyakula",amesema.

Amesema wanachama wa JOWUTA wataendelea kuwa mabalozi wa TPHPA na kuhabarisha umma juu ya majukumu ya mamlaka hiyo na manufaa yake makubwa kwa umma.

Juma alisema JOWUTA mwaka huu itashiriki maadhimisho na Mei mosi kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga na shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na inatarajiwa  kutoa wafanyakazi bora katika sekta ya habari.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com