Na mwandishi wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) ambaye ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wa Malawi Richard Chakupaleza Chikoko Luhanga anatarajiwa kufanya ziara rasmi ya siku nne nchini Tanzania kuanzia Aprili 20, 2026 akitarajiwa kupokelewa na Mwenyeji wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camilus Wambura.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amewaambia waandishi wa habari leo Jumatatu Aprili 20, 2025 Mkoani Dodoma kuwa ziara hiyo ni miongoni majukumu ya Mwenyekiti huyo anayeongoza kutembelea nchi wanachama kwa lengo la kukagua utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyopitishwa katika mkutano uliofanyika Jijini Dar Es Salaam Juni 2025.
"Wakati wa ziara hiyo kutafanyika kikao maalumu kitakacholenga kutoa taarifa ya utekelezaji wa maazimio kwa Mwenyekiti huyo wa SARPCCO ambapo miongoni hayo ni pamoja na kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa na ule unaovuka mipaka kwa lengo la kuzuia na kudhibiti matukio ya kihalifu katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika." Amekaririwa Kamanda Misime.
SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995 kwa dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya Majeshi ya Polisi katika nchi za Kusini mwa Afrika kwa lengo la kukabiliana na uhalifu wa kupangwa na unaovuka mipaka pamoja na kubadilishana taarifa na uzoefu katika kutekeleza majukumu ya Polisi.
Shirikisho hilo linaundwa na Nchi wanachama 16 ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Social Plugin