Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAWIA KUSHIRIKIANA NA MAIPAC MAADHIMISHO SIKU YA WAJANE, KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

Na Mwandishi wetu, Arusha 

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajane Tanzania (TAWIA), Rose Sarwatt ametembelea Ofisi za Taasisi ya Wanahabari ya usaidizi wa jamii  za pembezoni (MAIPAC)  kufanya mazungumzo juu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Wajene Tanzania ambayo yatafanyika Mkoa wa Kilimanjaro Juni 23 mwaka huu.

Siku ya Wajane Duniani inatambuliwa na Umoja wa Mataifa na Tanzania imekuwa ikiadhimishwa Kwa ushirikiano wa TAWIA na Serikali.

Akizungumza katika ofisi za MAIPAC jijini Arusha, Aprili 3, 2026, Sarwatt amesema maandalizi muhimu ya maadhimisho ya siku ya wajane yameanza.

Amesema maadhimisho Kitaifa yatafanyika Moshi mkoa wa Kilimanjaro na maadhimisho ya kidunia yatafanyika nchini Uingereza.

"Nimekuja MAIPAC kama mmoja wa mashirika ambayo yamekuwa yakifanya kazi na Wanawake wajane hasa kutoka jamii za pembezoni hivyo ni muhimu kushirikiana",amesema. 

Amesema TAWIA tayari imekuwa na ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro kufanikisha maadhimisho hayo.

"Ingawa tutashirikiana na Serikali nimeona kuna muhimu wa kushirikiana pia na  CSOs ambazo zimekuwa zikisaidia Wanawake kama nyie MAIPAC na wengine katika kufanikisha maadhimisho haya",amesema.

 Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu, licha ya kuwepo kongamano maalum pia wajane watapanda Mlima Kilimanjaro, wengine watatembelea hifadhi nyingine za Taifa", amesema Sarwatt.

Amesema bado TAWIA inaomba wafadhili wajitokeze kuwezesha maadhimisho haya ya kihistoria ambayo yatakutanisha zaidi ya wajane 500 nchi nzima.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma Siwayombe amesema  wapo tayari kushirikiana na TAWIA katika maadhimisho hayo.

Juma amesema MAIPAC imekuwa na miradi ambayo imeshirikisha Wajane katika wilaya za Monduli, Longido na Karatu hivyo kushiriki katika maadhimisho haya ni jambo muhimu.

"MAIPAC tunakuhakikishia ushirikiano mkubwa ikiwepo pia kushirikisha vyombo vya habari vingi katika maandalizi na maadhimisho ili kuongeza uelewa wa siku ya Wajane",amesema.

Naye Afisa Utawala wa MAIPAC, Andrea Ngobole amesema MAIPAC ambayo ina wanachama wanahabari zaidi ya 100 nchi nzima itatumia maadhimisho hayo kuhamasisha haki za Wajane na kuelezea umuhimu wa kuandika Wosia kwa wanafamilia ili kupunguza mgogoro baada ya mmoja wa wanafamilia kufariki dunia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com