
Na Mbuke Shilagi, Kagera.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Bukoba Mjini, James Michael Nyamanza, amewataka vijana kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na serikali ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza na Malunde 1 Blog, Nyamanza amesema kuwa fursa hizo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika awamu ya sita, zinazolenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Amebainisha kuwa mikopo hiyo inapatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Michezo pamoja na nyanja nyingine za kiuchumi, na kusisitiza umuhimu wa vijana kuitumia ipasavyo ili kuboresha maisha yao.
“Katika Wizara zote hizi, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya vijana kuomba mikopo kwa lengo la kujiendeleza,” amesema Nyamanza.
Aidha, Nyamanza amewakumbusha vijana kutokupuuzia fursa hizo pindi zinapojitokeza, bali wajitokeze kwa wingi kuomba na kunufaika nazo.
“Pia Wizara ya Vijana ilitoa tangazo ambalo lilikuwa linaisha tarehe tatu, lakini sasa tunapata taarifa kuwa maafisa vijana na wakuu wa Idara za jamii wanaojihusisha na vijana wameomba serikali kuongeza muda. Hivyo, tunatumia nafasi hii kuwakumbusha vijana kuwa fursa hizi zinapotangazwa wasiishie tu kusikiliza na kuziacha, bali wajitokeze kuomba. Fedha hizi zimeletwa kwa ajili ya vijana, na vijana wenyewe ndiyo sisi,” amesema Nyamanza.
Kwa upande wa upatikanaji wa fomu za maombi, Nyamanza amefafanua kuwa fomu hizo zinapatikana kwa urahisi kupitia njia mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii, stationary, pamoja na ofisi za kata zilizopo ndani ya Manispaa na Mkoa.
Amesisitiza kuwa hakuna sababu kwa vijana kukosa taarifa au kushindwa kuzipata fomu hizo endapo watakuwa na utayari wa kufuatilia kwa karibu.
Pia amewahimiza vijana kuwasiliana na Maafisa Maendeleo ya jamii waliopo katika maeneo yao, ambao wako tayari kutoa msaada wa namna ya kupata taarifa sahihi, kuandaa maandiko ya miradi pamoja na hatua zote muhimu za kufanikisha maombi ya mikopo hiyo.
''Naomba vijana wenzangu wafike kwenye ofisi za Maendeleo ya jamii waweze kuzungumza na Maafisa kwa ajili ya kupata uelewa na kusaidiwa namna ya kujaza fomu hizi za kwenye mitandao, kuanzia kuandika andiko la mradi kuandika barua lakini kutengeneza CV na kuziwasilisha kwenye mifumo'', amesema Comrade Nyamanza.
Social Plugin