Dkt. Egbert Mkoko kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwasilisha mada kuhusu uandishi wa habari unaojenga taifa badala ya kubomoa.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu na majukwaa yao kama nyenzo madhubuti ya kujenga taifa, kukuza amani na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, badala ya kusambaza maudhui yanayoweza kuligawa jamii, wakikumbushwa kuwa taifa hujengwa na simulizi zake, hivyo wanapaswa kusimulia hadithi zinazounganisha, kuelimisha na kuchochea ujenzi wa taifa.
Rai hiyo imetolewa na Dkt. Egbert Mkoko kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu uandishi wa habari unaojenga taifa badala ya kubomoa, katika kikao cha wadau wa sekta ya habari kilichofanyika Aprili 17, 2026 jijini Dar es Salaam.
Katika wasilisho lake, Dkt. Mkoko amesisitiza kuwa uandishi wa habari ni nguvu kubwa katika jamii inayoweza kuunganisha watu, kuimarisha demokrasia na kuchochea maendeleo; lakini pia inaweza kusababisha mgawanyiko, hofu na hata machafuko iwapo haitatumika kwa umakini.
Waandishi wanapaswa kufanya nini
Akizungumzia wajibu wa waandishi wa habari, Dkt. Mkoko amesema ni muhimu kuhakikisha ukweli wa taarifa kabla ya kuzichapisha, kutoa habari zenye uwiano na usahihi, pamoja na kuzingatia maadili na weledi wa taaluma hiyo.
Ameongeza kuwa waandishi wanapaswa kukuza amani kwa kuhamasisha mazungumzo chanya ndani ya jamii, huku wakielekeza nguvu zaidi katika kuibua suluhisho na kuonyesha mafanikio ya maendeleo badala ya kuangazia matatizo pekee.
Kwa upande mwingine, amewataka waandishi kujiepusha na kuchapisha taarifa bila uhakiki, kusambaza chuki au ubaguzi, pamoja na kuchochea migogoro kupitia maudhui yasiyo na uwajibikaji.
“Ni hatari kwa mwandishi kupotosha umma au kutumia uandishi wa kusisimua kupita kiasi (sensationalism), kwani hali hiyo inaweza kuharibu taswira ya vyombo vya habari na kuathiri utulivu wa taifa,” ameonya.
Akitolea ufafanuzi wa maudhui hatarishi, Dkt. Mkoko ametaja lugha za chuki, habari za uongo, upotoshaji, pamoja na simulizi zinazogawa jamii kuwa ni miongoni mwa mambo yanayoweza kulivuruga taifa.
Amesema madhara yake ni pamoja na kuzua vurugu na machafuko, kupotea kwa imani ya wananchi kwa vyombo vya habari, na kudhoofika kwa utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Mtazamo wa uandishi wa habari za maendeleo
Katika mtazamo wa uandishi wa habari za maendeleo, amewataka waandishi kuelekeza nguvu katika kuunga mkono ajenda za kitaifa, kuangazia fursa zilizopo na kushirikisha wananchi katika mijadala ya maendeleo.
“Uandishi wa habari haupaswi kuishia kuripoti matatizo bali utoe dira ya suluhisho na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo yao. Taifa hujengwa na simulizi zake; waandishi wanapaswa kusimulia hadithi zinazounganisha, kuelimisha na kujenga taifa,” amesisitiza.
Dkt. Mkoko amependekeza vyombo vya habari kuweka mikakati madhubuti, ikiwemo kuanzisha mifumo ya uhakiki wa taarifa (fact-checking), kuandaa miongozo ya kuripoti migogoro, pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa waandishi.
Aidha, ameeleza kuwa wahariri wana jukumu kubwa kama walinzi wa maudhui (gatekeepers), kuhakikisha taarifa zinazochapishwa zinafuata maadili na hazina athari hasi kwa jamii.
Kikao hicho cha wadau wa sekta ya habari kililenga kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kuhamasisha amani, utulivu, umoja wa kitaifa na maridhiano nchini.


Social Plugin