Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SEKTA YA MADINI YAZIDI KUIBUKA KINARA WA UWEKEZAJI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Sekta ya madini nchini imeendelea kuonesha mwelekeo chanya na kuimarika, huku ikiibuka kinara katika kuvutia Mtaji wa Uwekezaji wa Nje (FDI Stock), kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2025.

Waziri wa Madini, Antony Mavunde, ameeleza hayo wakati akiwasilisha Bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akisisitiza kuwa sekta hiyo imeendelea kuwa mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa taifa.

Amesema kuwa mwaka 2024, sekta ya madini ilifikia uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 9.79, ikiwa ni ongezeko kutoka dola bilioni 9.15 mwaka 2023 na dola bilioni 8.64 mwaka 2022. Takwimu hizi zinaonesha mwenendo thabiti wa ukuaji wa uwekezaji katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mafanikio hayo yanatokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuhamasisha wawekezaji wapya, pamoja na kupanua miradi iliyopo. Aidha, matumizi ya faida zinazozalishwa ndani ya sekta hiyo yameendelea kuchochea uwekezaji zaidi, hatua inayosaidia kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.

Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa na ya kihistoria katika kuendeleza madini muhimu na ya kimkakati, ikiwemo niobium, nikeli, grafaiti na dhahabu. Maendeleo hayo yamechangiwa na kusainiwa kwa mikataba mbalimbali ya utekelezaji wa miradi katika maeneo tofauti nchini.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kusainiwa kwa mkataba wa kuendeleza mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium wa Panda Hill, uliopo mkoani Mbeya, tarehe 24 Machi 2026. Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuongeza thamani ya madini, ajira kwa wananchi na pato la taifa kwa ujumla.

Ukuaji huu wa sekta ya madini unaendelea kuweka msingi imara wa Tanzania kunufaika zaidi na rasilimali zake, huku ukichochea maendeleo ya sekta nyingine za uchumi na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com