Jeshi la Polisi Mkoani Rukwa leo Jumatano Aprili 08, 2026 limetangaza kuwakamata Vijana saba katika Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa, wawili kati yao wakipandishwa Mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja, kwa kudai kuibiwa nyeti zao suala ambalo si kweli na lilichochea wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija amewaambia waandishi wa habari kuwa hatua hiyo imetokana na msako uliofanywa Aprili 06, 2026 kufuatia taharuki zilizosababisha vurugu na kukosekana kwa amani na utulivu wa jamii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoani Rukwa kutokana na baadhi ya watu kudai kuibiwa nyeti zao.
"Vijana wawili kati ya saba ambao ni Haruni Willium Mengo (24) Mkazi wa Kalambazile na Isack Simon Kaniki (19) mkazi wa Mshani wamefikishwa mahakamani na kuonekana na hatia na wote wawili wamepewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi sita jela kila mmoja." Amesema Kamanda Masija.
Kamanda Masija amebainisha kuwa adhabu hiyo imetolewa Aprili 08, 2026 na Mhe. Wiligisi Mbunda, Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Kipeta Wilayani Sumbawanga ambapo imeelezwa kuwa wakiwa kwenye Kijiji cha Mshani Wilayani Sumbawanga vijana hao walimzushia Bw. Issa Athuman Kidungwe (56) Mkazi wa Handeni Mkoani Tanga kuwa ameiba nyeti zao na hivyo Bw. Kidungwe kushambuliwa na kupigwa maeneo mbalimbali na kumsababishia maumivu makali.
"Watuhumiwa wengine watano wanaendelea kushikiliwa ambao ni Geofrey Dominic (24), Jafari Nebart (25) wakazi wa Kijiji Kilangawana, Huruma Kasonso (18), Mkazi wa Kilyamatundu, Constantino Kiatu (26) na Severino Ngonyani (22) Wakazi wa Sumbawanga ambapo taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao ili kufikishwa mahakamani.
Katika taarifa yake hiyo Kamanda Masija pia ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia inayoendelea ya kuzusha taharuki kwa jamii, akisisitiza pia wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, akihimiza pia wananchi kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi pale wanapobaini viashiria vya vurugu au uhalifu.

Social Plugin