Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA NI MAMA WA UVUMILIVU, HURUMA NA UPENDO KWA WOTE- MALATA



Mama na Baba lishe wa Tanzania wamemtaja Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama alama ya historia mpya katika historia ya Tanzania, akiwa rais wa kwanza Tanzania mwenye kubeba bendera ya matumaini, ujasiri na hekima isiyopimika, wakimtaja kama kinara wa uvumilivu, busara, upendo wa Kitaifa na Kiongozi mwenye Uongozi wa kuunganisha watanzania bila ubaguzi wowote.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mamalishe Tanzania UMALITA Bi. Julieth Malata wakati wa kongamano la Kitaifa la Mama Lishe na Baba lishe, kongamano ambalo linafanyika Jijini Dar Es Salaam, mgeni rasmi akiwa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya kaulimbiu isemayo "shiriki kulinda amani na mshikamano wa Taifa, amani ni hazina yetu Mama na baba lishe".

"Mhe. Rais wewe si tu Kiongozi bali pia mwalimu wa Taifa na kizazi kijacho ambapo kupitia mikono yako imara taifa limepiga hatua kubwa kiuchumi, diplomasia, uwezeshaji wa mwanamke, vijana na wajasiriamali wadogo huku ukionesha kwa vitendo kuwa mwanamke anaweza kuongoza kwa mafanikio makubwa zaidi pale anapopewa nafasi." Amesema Bi. Malata.

Kiongozi huyo pia amebainisha kuwa UMALITA wanamtazama Rais Samia kama dira ya mafanikio yao, wakijifunza kutoka kwake Mama jasiri, mwenye maono, subra na uthubutu wa kufanya maamuzi magumu kwa maslahi ya Taifa, wakisema Rais Samia mara zote amewapa nguvu Mama na Baba lishe ya kufikia ndoto kubwa katika kujenga biashara zenye hadhi na ubora, wakiamini kuwa hata katika mazingira magumu mafanikio yanawezekana.

"Wewe ni mwanga unayeangaza maisha yetu, ni mfano wa kuwa mwanamke anayeweza kubeba taifa, kuleta heshima na kuacha alama ya milele ya maendeleo, umoja na ustawi wa Watanzania wote, ukiwa chanzo cha uhai, huruma, uvumilivu, upendo usio na mipaka na uwezo wa kujitoa kwaajili ya ustawi wa wengine bila kujali changamoto." Ameongeza kusema.

Malata pia amemshukuru Rais Samia kwa mageuzi yake makubwa kwa kuboresha mazingira yao ya kazi ikiwemo hamasa yake ya matumizi ya nishati safi suala ambalo limeokoa maisha ya Mama na Baba lishe wengi waliokuwa wakikumbwa na magonjwa ya mifumo ya upumuaji, akiutaja mchango huo kuwa wa kiutu na ushahidi wa uongozi wenye kujali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com