Kaimu mkurugenzi wa BOT kanda ya Mwanza Amon Mwambonda akizungumza wakati wa mafunzo ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).
Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani humo yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).
Na Mwandishi Wetu - Kahama
Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kutumia mifumo rasmi ya malipo ili kuongeza usalama wa fedha zao, kuboresha biashara na kujijengea historia ya miamala itakayorahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Akizungumza katika mafunzo ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Latifah Mikoyi kutoka BOT, anayesimamia mifumo ya malipo amesema, matumizi ya mifumo rasmi ya malipo hupunguza utegemezi wa fedha taslimu.
Amesema mifumo hiyo pia inaondoa hatari ya wizi, upotevu na changamoto nyingine za usalama.
Amesema kupitia teknolojia ya kifedha, wachimbaji wanaweza kufanya miamala kwa kutumia simu za mkononi, huduma za kibenki kwa njia ya simu (mobile banking) pamoja na njia nyingine za kidijitali bila ulazima wa kubeba fedha taslimu.
“Mfumo wa malipo unamsaidia mchimbaji kupokea malipo kwa haraka kutoka kwa wanunuzi wa madini, kulipa wafanyakazi kwa urahisi na kuepusha matumizi ya cash ambayo yanaweza kuwa na hatari,” alisema Mikoyi.
Mikoyi amesema matumizi ya mifumo rasmi ya malipo huwasaidia wachimbaji kujenga rekodi za kifedha, jambo ambalo ni muhimu wanapotaka kuomba mikopo kwenye benki na taasisi nyingine za fedha.
“Wachimbaji wengi wanakosa mikopo kwa sababu hawana taarifa rasmi za biashara zao, kwani hutumia cash pekee. Wakianza kutumia mifumo rasmi ya malipo, miamala yao itaonekana na itawasaidia kukopesheka,” aliongeza.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mukrim Ramadhan kutoka BOT, amesema Taifa lenye wananchi wenye uelewa mkubwa wa masuala ya fedha, lina nafasi kubwa ya kufikia maendeleo ya haraka na endelevu.
“Tunataka wananchi wetu waweze kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kutumia mapato yao kwa tija, lakini pia kuona fursa zilizopo za uwekezaji,” alisema Ramadhan.
Amesema kuwa Benki Kuu imeanzisha mtaala na programu maalumu ijulikanayo kama Certified Financial Educator, inayolenga kuwathibitisha wataalamu wanaotoa elimu ya fedha nchini.
Amesema kupitia programu hiyo, zaidi ya watu 1,050 kutoka maeneo mbalimbali nchini wameidhinishwa kuwa wakufunzi wa masuala ya fedha, ambapo wamekuwa wakifika kwenye jamii na kutoa elimu hiyo kwa wananchi.
Ramadhan ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayosisitizwa katika mafunzo hayo ni uwekezaji, ikiwemo kutumia fursa zinazotolewa na Benki Kuu kama Bonds za Serikali, ambazo ni njia salama ya kukuza mitaji na kuweka akiba yenye tija.
Katika mafunzo hayo, mchambuzi wa masuala ya fedha kutoka BOT, CPA Michael Israel Mwaituka, alieleza pia kuhusu uwepo wa mifuko ya dhamana ya mikopo (Credit Guarantee Schemes) iliyoanzishwa na Serikali kusaidia wajasiriamali na wachimbaji kupata mitaji.
Amesema mifuko hiyo ni pamoja na Export Credit Guarantee Scheme ulioanzishwa mwaka 2012/2013 kwa ajili ya kuchochea mauzo nje ya nchi, pamoja na mfuko wa dhamana kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ulioanzishwa mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mwaituka, kupitia mifuko hiyo BOT inaweza kutoa dhamana kwa wachimbaji wanaohitaji mikopo ya kununua vifaa vya uchimbaji au kuendeleza shughuli zao, jambo litakalowasaidia kupata fedha kutoka taasisi za kifedha kwa urahisi zaidi.
Naye Benedict Toto kutoka chemba ya Taifa ya biashara, viwanda na kilimo Tanzania (TNCCIA), amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mikopo, haswa kutokana na gharama kubwa za vifaa vinavyohitajika katika shughuli za uchimbaji.
Kutokana na hali hiyo, ameishauri BOT na benki za biashara kupitia upya sera za mikopo ili ziendane na mazingira na mahitaji halisi ya wachimbaji wadogo nchini.
Amesema “Wachimbaji wadogo wanahitaji vifaa vya gharama kubwa ili kufanya kazi kwa ufanisi, lakini mara nyingi sera za mikopo zilizopo katika benki za biashara hazikidhi mahitaji yao.”
Wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta hiyo Wilayani Kahama wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kubadili mtazamo wa matumizi ya fedha, kuweka akiba na kuwekeza kwa manufaa ya baadaye.
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), Gregory Kibusi, amesema elimu hiyo ni muhimu kwani imejikita katika maeneo muhimu kama utunzaji wa fedha, kupanga bajeti, kuwekeza na namna ya kukidhi vigezo vya kupata mikopo.
“Wachimbaji wengi wamekuwa wakilalamika kukosa dhamana za mikopo. Leo wameelezwa kuwa wanaweza kuwekeza kwenye UTT, Treasury Bonds na hatifungani nyingine ambazo zinaweza kutumika kama dhamana ya kukopesheka kwa haraka,” amesema Kibusi.
Mchimbaji mdogo Solomon Mataba amesema changamoto kubwa kwa wachimbaji wengi ni kutumia fedha bila mipango baada ya kupata mapato makubwa.
Amesema “Mtu anaweza kupata hata milioni mia mbili, lakini baada ya wiki mbili au mwezi mmoja hana hata fedha ya matumizi ya kawaida. Mafunzo haya yatatusaidia kujua namna ya kutumia fedha na kuweka mipango ya maisha.”
Naye Irene Msuya, mchimbaji mdogo kutoka kampuni ya Kilosa Kwe, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kuvunja hofu kuhusu huduma za benki na mikopo.
Amesema “Watu wengi walikuwa wanaamini ukienda benki ni vigumu kupata huduma. Lakini sasa tumejifunza kuwa tunaweza kupanga mapato yetu, kuweka akiba na hata kukopesheka.”
Awali akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Kahama kufumgua mafunzo hayo, kaimu mkurugenzi wa BOT kanda ya Mwanza Amon Mwambonda alieleza kuwa mifumo hiyo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya BOT katika kipindi cha miaka 60.
“Kumetokea mageuzi makubwa sana kwenye mifumo ya malipo, yamerahisishwa sana, na sisi BOT tunalisimamia kuhakikisha watu wanapata huduma za malipo za haraka na zilizo salama.” Amesema Mwambonda
Akifungua mafunzo hayo, mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, (BOT) kwa kuandaa mafunzo hayo na kwamba ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Amesema ili wananchi wafikie maendeleo ya kweli ni lazima wawe na uelewa wa masuala ya fedha na namna bora ya kutumia rasilimali walizonazo.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa wananchi, kuboresha ustawi wa familia na kujenga taifa lenye nguvu kiuchumi.
“Kwa kufikia maendeleo tunayoyataka lazima tuwe na elimu ya fedha katika jamii. Hili ni wazo zuri sana na tunawapongeza BOT kwa kuchagua Wilaya ya Kahama kwa mafunzo haya muhimu,” amesema Nkinda.
Aidha amesisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kubadilisha maisha ya wachimbaji na familia zao, huku akieleza matumaini kuwa maarifa yatakayopatikana yatachochea mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika jamii ya Kahama na maeneo jirani.
Latifah Mikoyi kutoka kurugenzi ya mifumo ya malipo BOT, akizungumza na wanahabari baada ya mafunzo ya elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).

Muwezeshaji wa mafunzo ya elimu ya elimu ya fedha kwa wachimbaji Mukrim Ramadhan kutoka chuo cha benki kuu ya Tanzania (BOT), akitoa elimu hiyo kwa wachimbaji katika mafunzo yaliyoandaliwa na BOT.
Benedict Toto kutoka chemba ya Taifa ya biashara Tanzania (TNCCIA), akizungumza na wanahabari baada ya mafunzo ya elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).
Mchambuzi wa masuala ya fedha kutoka BOT, CPA Michael Israel Mwaituka akizungumza na wanahabari baada ya mafunzo ya elimu kwa wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama mkoani Shinyanga yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).
Baadhi ya wachimbaji wadogo na wa kati wilayani Kahama wakiwa ukumbini katika mafunzo ya elimu ya fedha kwao, yaliyoandaliwa na benki kuu ya Tanzania (BOT).



















Social Plugin