Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NSSF YAFIKIA TRILIONI 11.2, WAZIRI SANGU ABAINISHA HIFADHI SKIMU INAVYOENDA KUBADILI MAISHA YA WATANZANIA

Na MWANDISHI WETU, Dodoma.

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarika kwa kasi, ukifikia thamani ya shilingi trilioni 11.2 hadi Machi 2026 kutoka trilioni 4.3 mwaka 2020, hatua inayoakisi ukuaji wa uwekezaji, uimara wa usimamizi na kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi kupitia Hifadhi Skimu.

Ukuaji huo umeambatana na upanuzi wa huduma za hifadhi ya jamii, hususan kupitia hifadhi skimu zinazolenga kuwafikia wananchi waliojiajiri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza wigo wa wanachama na kuimarisha ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya jamii katika mfumo wa hifadhi ya jamii.

Akizungumza jijini Dodoma tarehe 27 Aprili 2026 wakati akifungua Mkutano wa 56 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, alisema mafanikio ya Mfuko yanatokana na mageuzi ya usimamizi, uwekezaji wenye tija na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.

Alisisitiza kuwa hifadhi skimu ni nguzo muhimu ya mustakabali wa hifadhi ya jamii nchini, akibainisha kuwa Serikali inalenga kuhakikisha Watanzania wengi zaidi, hususan waliojiajiri, wanajumuishwa katika mfumo huo.

“Upanuzi wa hifadhi skimu ni hatua muhimu ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nje ya mfumo wa hifadhi ya jamii,” alisema Mhe. Sangu.

Waziri huyo pia aliipongeza NSSF kwa mchango wake katika uchumi wa taifa kupitia uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayozalisha ajira na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, akitaja kiwanda cha sukari cha Mkulazi kuwa mfano wa uwekezaji wenye tija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti wa fedha, uwekezaji salama na matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyofikia takribani asilimia 99 ya huduma.

Alisema katika Mpango Mkakati wa miaka mitano (2026/27–2030/31), NSSF inalenga kufikia thamani ya shilingi trilioni 24.7 ifikapo Juni 2031, pamoja na kuongeza wanachama hadi milioni 6.6, huku mkazo ukiwekwa katika kuimarisha mpango wa Hifadhi Skimu na kuzingatia misingi ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG). Katika kupata hati safi za ukaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mafanikio hayo yametokana pia na Mfuko kufuata misingi ya utawala bora, uwazi, uwajibikaji na uwekezaji wenye tija, hali inayoendelea kuimarisha imani ya wadau na umma kwa ujumla.

Pamoja na mafanikio hayo, Mfuko unaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya waajiri kutowasilisha michango kwa wakati, kuwasilisha michango chini ya kiwango halisi, pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya hifadhi ya jamii kwa baadhi ya makundi ya wananchi, hali inayopatiwa ufumbuzi kupitia elimu na uhamasishaji unaoendelea.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira bora na wezeshi ya ufanyaji kazi, uwekezaji pamoja na biashara, jambo lililochochea ongezeko la wanachama na uimara wa mifumo ya hifadhi ya jamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu alieleza kuwa mipango ya Mfuko inaendana kikamilifu na mipango mikuu ya Serikali ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 na Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii. Alisema Serikali inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2050, takribani asilimia 70 ya Watanzania watakuwa wamefikiwa na mifumo ya hifadhi ya jamii kupitia upanuzi wa Hifadhi Skimu na mifumo jumuishi ya kinga ya kijamii.

Waziri huyo alisema mafanikio ya sekta hiyo ni sehemu ya mwelekeo mpana wa taifa wa kujenga uchumi shirikishi unaomlinda kila Mtanzania.

Mkutano huo wa 56 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF unajadili Mpango Mkakati wa Nane pamoja na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, likiwa ni jukwaa muhimu la kuweka mwelekeo wa baadaye wa Mfuko na mustakabali wa hifadhi ya jamii nchini.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com