Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WADAU WAKUTANA KUZUNGUMZIA MRADI WA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE WA KIMATAIFA CHA SERENGETI

Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Jumapili April 20, 2026 wamekutana na wadau mbalimbali kuzungumzia mipango ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Serengeti ambao unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayobadilisha taswira ya sekta ya usafiri wa anga na utalii nchini Tanzania. 

Kikao hicho kilifanyika katika Mugumu ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, kikilenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu maendeleo na hatua za utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga pamoja na kukuza utalii nchini.

Mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa kupokea ndege za kimataifa moja kwa moja, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa watalii pamoja na wawekezaji, na hivyo kukuza uchumi wa taifa

Katika kikao hicho walikuwepo pia PSSSF, uongozi wa Halmashauri ya Serengeti pamoja na kampuni ya Saba Engineering, ambayo ni mshauri elekezi anayesimamia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu, Bw. Shomari Shomari, amesema Wizara inatambua umuhimu wa mradi huo na imejipanga kuhakikisha unatekelezwa kwa wakati kama ulivyopangwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Abdul Mombokaleo, amesisitiza kuwa mradi huo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa, hasa katika kukuza utalii wa Hifadhi ya Serengeti, ambayo ni moja ya vivutio vikuu duniani. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijamii na kimazingira ili kuhakikisha wananchi wa maeneo husika wananufaika ipasavyo na mradi huo.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iko kaskazini mwa Tanzania, ikienea kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wa Mara, huku sehemu zake zikigusa pia mikoa ya Simiyu na Arusha. 

Hifadhi hii ni maarufu duniani kwa uhamaji mkubwa wa wanyama, hususan zaidi ya nyumbu milioni 1.5 wanaohama kila mwaka wakifuatiwa na pundamilia na swala. Serengeti pia ni eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, na ni moja ya vivutio vikuu vya utalii nchini, likivutia wageni kutoka kote duniani kutokana na wingi na utofauti wa wanyamapori wake.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com