Mwenyekiti wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania (VIWAWA), Leonard Mapolu, amewahimiza vijana nchini kuthamini na kulinda amani iliyopo pamoja na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Mapolu amesema muungano huo ni alama muhimu ya mshikamano wa Watanzania na unapaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani umeendelea kuwa chachu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameonya kuwa jitihada zozote za kuvuruga amani zinapaswa kupuuzwa na kukemewa kwa pamoja, akieleza kuwa wanaofanya hivyo hawana nia njema kwa taifa.
Akizungumzia umuhimu wa amani, Mapolu ameeleza kuwa amani huanza kwa mtu binafsi katika maisha ya kila siku, hususan katika utoaji wa huduma.
Amesisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kutenda haki na kuwajibika ipasavyo ili kudumisha mazingira ya utulivu katika jamii.
Aidha, amesema uzoefu wake wa kutembelea maeneo mbalimbali nchini kupitia shughuli za utume umemuwezesha kushuhudia kwa karibu namna ambavyo amani inavyorahisisha utekelezaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi.
Amebainisha kuwa bila uwepo wa amani, isingekuwa rahisi kufikia na kuhudumia jamii katika maeneo tofauti.
Mapolu amewasihi vijana kutambua nafasi yao kubwa katika kulinda amani ya nchi, akieleza kuwa wao ni nguvu kazi ya taifa na wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha utulivu unaendelea kudumu.
Aidha, amewatahadharisha dhidi ya kurubuniwa au kutumiwa vibaya na watu wenye nia ya kuvuruga amani.
Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa vijana kujenga mshikamano, kuheshimiana na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Ameeleza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji utulivu, ushirikiano wa wananchi pamoja na maridhiano ya dhati.
Mapolu ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuilinda amani ya nchi kwa nguvu zote, akibainisha kuwa amani ni tunu adhimu inayopaswa kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Social Plugin