Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, ametoa wito mzito kwa vijana na wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu nchini kusimama imara katika kulinda, kutetea, na kuendeleza misingi ya Muungano.Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua kongamano maalumu la kumuenzi muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Shehe Abeid Amani Karume, Waziri Masauni alisisitiza kuwa umoja uliopo sasa ni matokeo ya maono na dhabihu kubwa zilizotolewa na waasisi wetu kwa ajili ya mustakabali wa vizazi vyote.
Katika kumuelezea Shehe Karume, Waziri Masauni alimtaja kama kiongozi shujaa na mwenye maono ya kipekee ambaye alijipambanua kwa kutetea maslahi ya wanyonge na kuweka misingi imara ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alibainisha kuwa sera za kihistoria kama ugawaji wa ardhi, elimu na matibabu bure, pamoja na ujenzi wa makazi ya kisasa, ni alama zisizofutika zinazoonyesha jinsi kiongozi huyo alivyogusa maisha ya wananchi.
Karume alitajwa kama muumini wa kweli wa uanamajumui wa Kiafrika aliyeweza kuunganisha mataifa ya Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo ili kuleta amani na nguvu ya pamoja.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Richard Muyungi, alieleza kuwa kongamano hilo ni mwanzo wa juhudi za kimkakati za kuwafikia vijana wa Tanzania Bara ili kuwajengea uelewa wa kina kuhusu historia ya nchi yao.
Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa mchango wa waasisi hausahauliki na badala yake unatumika kama dira ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Kupitia mijadala hiyo, vijana wanahimizwa kuwa walinzi wa amani na kielelezo cha umoja unaoifanya Tanzania kuwa mfano bora wa ushirikiano barani Afrika na duniani kote.
Social Plugin