Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKOYE NA KISAKA WAKAMATWA KWA KUZUSHA ‘WAMEPOTEZA SEHEMU ZA SIRI’ KAHAMA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata watuhumiwa wawili (Kisaka Elinihaki na Makoye James) kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kuhusu kupoteza sehemu zao za siri, hali iliyosababisha taharuki kubwa miongoni mwa wananchi katika Wilaya ya Kahama.

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 7, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kamanda Magomi amesema tukio la kwanza lilitokea Aprili 4, 2026 katika Soko Kuu lililopo eneo la Stendi Kuu ya Mabasi, Kata ya Kahama Mjini, ambapo mwaume mmoja aitwaye Kisaka Elinihaki (22), mkazi wa Majengo, alidai kupoteza sehemu zake za siri kimiujiza baada ya kuguswa bega la kushoto na dereva mmoja aitwaye Joseph Godfrey (36), mkazi wa Shunu.

Amesema taarifa hiyo ya uongo ilisababisha taharuki kubwa kwa wananchi waliokuwepo eneo hilo, ambapo baadhi yao walichukua sheria mkononi na kuanza kumshambulia mtuhumiwa Joseph Godfrey wakimtuhumu kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi lilifika kwa haraka na kumwokoa mtuhumiwa huyo pamoja na kumchukua Kisaka kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Baada ya kufikishwa hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu, ilibainika kuwa mhusika hakuwa na madhara yoyote, na madai yake hayakuwa ya kweli. Kutokana na hali hiyo, tulimkamata kwa kosa la kutoa taarifa za uongo zilizoweza kuhatarisha usalama wa jamii,” amesema Kamanda Magomi.

Aidha, tukio la pili lilitokea Aprili 6, 2026 katika eneo la machimbo ya dhahabu Mwime, wilayani Kahama, ambapo kijana mmoja aitwaye Makoye James alitoa taarifa ya uongo akidai kupoteza sehemu zake za siri baada ya kushikwa na abiria mwenzake alipokuwa akisafiri kwa pikipiki.

Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, taarifa hiyo pia ilisababisha mkusanyiko wa wananchi waliokuwa na hasira, wakitaka kumshambulia mtu aliyekuwa akituhumiwa kabla ya Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio na kudhibiti hali hiyo.

“Uchunguzi wa kitabibu uliofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ulibaini kuwa mhusika hakuwa na tatizo lolote, hivyo kuthibitisha kuwa taarifa aliyotoa ilikuwa ya uongo. Naye amekamatwa na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yake,” alisisitiza.

Kamanda Magomi ameeleza kuwa vitendo vya kutoa taarifa za uongo vina madhara makubwa kwa jamii kwani vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani, madhara kwa watu wasio na hatia, na hata kupoteza maisha.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuzua taarifa zisizo na ukweli na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola katika kudumisha amani na usalama.

“Tunawaasa wananchi kuwa watulivu na kuepuka kuchukua sheria mkononi. Pale wanapopata taarifa yoyote yenye shaka, watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kusisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kusambaza taarifa za uongo zinazoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com