Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MARIDHIANO YATALIPONYA TAIFA NA KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO- SHEIKH JALALA



Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithnaasharia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemedi Jalala ameipongeza Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisema baada ya kuisikiliza ripoti ya Tume hiyo anaamini kuwa mapendekezo yake yanaenda kuondoa tofauti na changamoto za sasa na kurejesha umoja wa Kitaifa.

Sheikh Jalala ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 27, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, akimpongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza mchakato wa maridhiano Nchini, akisema kuwa maridhiano ndiyo yatakayotibu tofauti zote na majeraha mbalimbali kwa makundi tofauti ya kijamii na kisiasa.

"Kwakweli tayari tumepita kwenye matatizo, kwenye changamoto, sasa hivi muhimu ni kuangalia namna gani tunalirudisha taifa kwenye hali yake ya kawaida, namna gani watanzania wanarudi kwenye mshikamano, kwenye umoja wao wa Kitaifa na kwenye nchi yao ambayo ni kisiwa cha amani." Amesema Sheikh Jalala.

Kiongozi huyo wa dini amekumbusha pia umuhimu wa Viongozi wa dini nchini kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri amani na maridhiano kwa waumini wao, akisema kuwa ikiwa yatatekelezwa yote yaliyosemwa katika ripoti ya Tume ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande pamoja na kila mmoja kushiriki kwenye mchakato wa maridhiano, Taifa litabakia kuwa salama, lenye amani na mshikamano kwa kila mmoja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com