Kamati ya Maridhiano mkoani Shinyanga imelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kwa juhudi zake za kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, hususan katika kipindi hiki ambacho kumeibuka uvumi unaosababisha taharuki miongoni mwa wananchi ukidai kuwa mtu akiguswa begani hupoteza sehemu zake za siri kwa wanaume.Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano,amani, mila na desturi mkoani humo, Shekhe Balilusa Khamis, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, akiwa ameambatana na viongozi wengine wa dini mbalimbali, Mkuu wa Machifu pamoja na Kamanda wa Vikundi vya Ulinzi Shirikishi. Amesema kuwa juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza hofu kwa wananchi na kurejesha hali ya utulivu katika jamii.
Aidha, Shekhe Khamis ametoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa zisizo na ukweli na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii. Ameongeza kuwa umoja na mshikamano wa viongozi wa dini na kimila ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na utulivu.
Kwa upande wake, Mtemi Kidola wa II ambaye ni Mwenyekiti wa Machifu mkoani Shinyanga, amempongeza Kamanda wa Polisi wa mkoa huo pamoja na wasaidizi wake kwa hatua wanazochukua dhidi ya watu wanaosambaza uvumi huo. Amesema kuwa kuwafikisha mahakamani wanaozusha taarifa hizo ni njia sahihi ya kukomesha upotoshaji unaoweza kusababisha taharuki na vurugu zisizo za lazima.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi ili kuondoa hofu isiyo na msingi na kuimarisha mshikamano wa kijamii mkoani Shinyanga.



Social Plugin