Na mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amegawa mitungi ya gesi kwa mama na baba lishe ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Tukio hilo limefanyika Leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026 likiwa ni sehemu ya Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe lililowakutanisha wajasiriamali wa sekta ya chakula kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kulinda afya za wananchi na mazingira, huku akieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.
Amebainisha kuwa matumizi ya gesi yatasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambao umechangia uharibifu wa mazingira na changamoto za kiafya, hususan kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za upishi.
Mama na baba lishe walionufaika na mpango huo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema itarahisisha shughuli zao za kila siku, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi katika huduma wanazotoa kwa wateja.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuendeleza matumizi ya nishati safi, huku ikiendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo ambao ni mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi.



Social Plugin