Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HAKUNA UTAJIRI MKUBWA ZAIDI YA UPENDO, UMOJA NA MSHIKAMANO- ASKOFU DKT. MAASA



Na mwandishi wetu, Arusha

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na amani Tanzania (JMAT) Baba Askofu Dkt. Maasa Ole Gabriel, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa busara na hekima zake zilizoifanya Tanzania kuendelea kuwa salama na yenye amani pamoja na kuanzisha mchakato wa maridhiano kwa kuunda Tume ya kushughulikia chanzo cha matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Askofu Dkt. Maasa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 03, 2026 kwenye Ofisi za Jumuiya hiyo Jijini Arusha wakati huu ambapo Taifa likisubiri siku chache kabla ya Rais Samia kukabidhiwa ripoti ya Tume iliyochunguza matukio hayo ya uvunjifu wa amani, akisisitiza Watanzania kuendelea kuwa watulivu pamoja na kudumisha amani na mshikamano uliopo nchini.

"Rais atakabidhiwa ripoti ambayo mawazo ya makundi mbalimbali yaliyoguswa na matukio ya Oktoba 29 wakiwemo Vijana, Viongozi wa dini na siasa pamoja na wanajamii wengine. Sisi Jumuiya ya maridhiano tunaendelea kusisitiza umuhimu wa utajiri wetu mkubwa tulionao wa amani, upendo, mshikamano, utulivu na upendo tulionao kama Watanzania. Niwaase Watanzania wenzangu kudumisha mambo haya, Rais Akabidhiwe ripoti hiyo, apitie hayo mawazo yetu na baadae tusubiri hatua za ziada." Amesisitiza Askofu Maasa.

Amebainisha kuwa kando ya utajiri wa maliasili nyingine ikiwemo gesi, madini, mafuta na mbuga za wanyama, hakuna Taifa linaloweza kufaidi rasilimali hizo bila ya uwepo wa amani na utulivu- akitoa rai kwa kila Mtanzania kujifunza kwa Mataifa mengine duniani na kuona umuhimu wa kuitunza amani kwa maslahi ya ustawi na maendeleo.

Katibu Mkuu huyo wa JMAT amezungumzia pia mchakato wa maridhiano, akieleza kuwa kutofautiana kwa wanajamii ni jambo la kawaida kama ilivyo kwa wakristo, waislamu na Viongozi wa Kimila wanaounda Jumuiya ya maridhiano, akiwasihi wanasiasa kuridhiana katika tofauti walizonazo pamoja na kutumia tofauti zao vyema katika mbio zao za kutafuta mamlaka pamoja na kudumisha na kuipa amani kipaumbele katika shughuli zao.

Dkt. Maasa akirejea maandiko Matakatifu kutoka katika Vitabu vya dini ya Kikristo na Kiislamu kuhusu umuhimu wa amani na umoja, amehimiza pia Vijana kutumia vyema mitandao ya kijamii na kujiepusha na uchochezi na tabia za kigeni kutoka kwenye mitandao ya kijamii, akiwataka kuwa mstari wa mbele katika kulinda maadili ya Kitanzania sambamba na kujiepusha na vyote vyenye kuhatarisha amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com