Na. Anita Allyfaksadi, Ofisi ya Rais - Utumishi
Wataalamu wa Utawala wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu nchini wanatarajiwa kukutana jijini Arusha kuanzia Mei 5 hadi 8, 2026 katika Mkutano Mkuu wa Pili wa mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Utawala wa Umma na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Barani Afrika (AAPAM) Tawi la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa AAPAM Tanzania Chapter, Bi. Leila Mavika, alisema mkutano huo utafanyika jijini Arusha ukiwaleta pamoja wataalamu wa kada hiyo ili kujadili namna ya kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Bi. Mavika, mkutano huo unalenga kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili katika utendaji kazi na kubaini fursa za kuboresha usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala katika utumishi wa umma.
Aliongeza kuwa mkutano huo utaongozwa na wataalamu wabobezi watakaowasilisha mada mbalimbali za kitaaluma zitakazochochea maboresho ya utendaji na kuongeza tija katika taasisi za umma.
Katika mkutano huo, Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), ambaye anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwataka waajiri kutoka wizara, taasisi za umma, mamlaka za serikali za mitaa na vyuo vikuu kuwawezesha watumishi wao kushiriki mkutano huo ili kuongeza ujuzi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Katika hatua nyingine, washiriki wa mkutano huo watapata fursa ya kushiriki zoezi la kuimarisha mshikamano (team building) litakalofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro siku ya mwisho ya mkutano huo.
Alisema mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kufikiri upya utoaji wa huduma kwa Umma: Jinsi Serikali inavyoweza kutumia Teknolojia kuanzisha huduma bora na zinazolenga wananchi, kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana na changamoto za mazingira.”
Jumuiya ya AAPAM ilianzishwa mwaka 1971 kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kiutendaji katika utawala wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu barani Afrika, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanachama wake.



Social Plugin