Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARRICK NORTH MARA YAWEZESHA VIJANA TARIME KUANZISHA MIRADI YA KIUCHUMI


Vijana wakiwezeshwa kuendesha miradi mbalimbali ikiwemo ya kilimo wataweza kujikwamua kiuchumi kama wanavyoonekana vijana wakiwa shambani kwenye mradi wa kilimo cha mboga wa Matongo unaofadhiliwa na Barrick North Mara (Picha kutoka maktaba)
Mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime katika mkoa wa Mara umeendelea kutekeleza moja ya sera ya mkakati endelevu wa kampuni ya kuwezesha wananchi wanaoishi jirani na migodi yake kuwa na maisha bora ambapo kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) umetoa shilingi milioni 220 kwa vikundi 13 vya vijana ili kuanzisha miradi ya kiuchumi katika vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi huo.

Hatua hii ni mwendelezo wa mgodi wa Barrick North Mara kuwezesha kiuchumi makundi mbalimbali katika jamii hususani vijana ambapo mwaka jana iliunga mkono jitihada za Serikali za kuwapatia leseni za uchimbaji ambapo mgodi ulitoa leseni zake na kufadhili mafunzo ya vijana hao zaidi ya 1700 wanaojiandaa kuingia katika uchimbaji wa madini chini ya programu ya Mining For a Brighter Tomorrow (MBT) inayolenga kuboresha usalama, kuongeza tija na kuondoa uvamizi wa mgodi kwa kuwapatia rasmi maeneo ya uchimbaji.

Tayari vikundi hivyo vimepokea fedha hizo, ikiwa ni ruzuku ya (CSR) ya mwaka uliopita kutoka kwa mgodi huo ambao unaendeshwa kwa ubia na serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jami wa Halmashauri hiyo, Anthony George Nyange amesema kuwa fedha hizo zimesaidia vijana takriban 100 wanachama wa vikundi hiyo kuanzisha miradi ya mbalimbali ya kiuchumi.
Anthony George Nyange

“Nawashukuru sana Barrick North Mara hususan idara ya mahusiano ya jamii kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa katika kufanikisha mpango huu wa ruzuku ya uwajibikaji kwa jamii kwa vijana,” amesema Nyange.

Nyange amesema miradi hiyo imesaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa katika vijiji hivyo kwa ajili ya ustawi wa jamii vinavyouzunguka mgodi huo.

“Wanufaika wengi ni vijana na wamejielekeza kwenye miradi ambayo siyo tu kwa ajili ya kujipatia kipato bali pia kutatua changamoto zilizokuwepo,” amesema.

Ametaja vikundi ambavyo vimenufaika na mpango huo kuwa ni Mokarambe Agribusiness, Hope and Revolution of Economy for Youth, Tunza Mazingira Nyamongo, Amshana Nyamongo na REMHOCHI.

Vingine ni Kazi ni Moyo, Konna Nne, Kiumanya, Ibuka Umoja, Tunaweza Kerende, Nyasa Group, Mtazamo Youth na Kikundi cha Keryoba.

Amesema baadhi ya vikundi hivyo vimeanzisha miradi ya usafi wa mazingira jambo ambalo limesaidia kuweka mji mdogo wa Nyamongo katika hali nzuri ya usafi na mazingira.

“Kwa mfano, kulikuwa na changomoto ya usafi katika mji wa Nyamongo, sasa hali ya usafi ni nzuri kwa sababu kuna kikundi cha mazingira ambacho kinafanya vizuri sana kwenye usafi wa mazingira,” amesema Nyange.

Nyange amesema Halmashauri ya Wilaya ya Tarime itaendelea kutenga sehemu ya fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi.

“Tunategemea na mwaka huu pia tutatenga sehemu ya CSR kwenda kuwezesha vijana kwenye miradi ya kiuchumi. Sasa hivi, vijana wengi kule Nyamongo wana shughuli za kufanya kujipatia kipato na hata vitendo vya kihalifu vimepungua,” amesema Nyange.

Amesema mbali na mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), vijana hao pia wamenufaika na mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na halmshauri hiyo kuwezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Wanufaika wakubwa ni vijana, na mbali ya kunufaika na mikopo yetu ya halmashauri ya asilimia 10, pia wamenufaika na mpango wa ruzuku ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa vijana,” amefafanua Nyange.

Taarifa zinaonesha Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inaongoza kwa kutoa kiasi kikubwa cha mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Mara.

Mgodi wa Barrick North Mara pamoja na kutekeleza sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) pia utoaji wa leseni za uchimbaji kwa vijana uliwezesha na mafunzo ya siku 14 yaliyofanywa kwa kushirikiana na serikali.

Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha sekta ya madini iankuwa na tija zaidi kwa kuzingatia usalama mahali pa kazi na utunzaji wa mazingira , usimamizi wa biashara za madini na kufuata sheria za nchini na usimamizi wa vikundi pamoja na elimu ya masuala ya fedha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com