
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amevaa sare za Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) mara baada ya kukabidhi mitungi ya gesi na majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026.
***
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa amani ni msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini, akisisitiza kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika kwa ufanisi.
Akizungumza Aprili 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kazi kwa Mama na Baba lishe ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija zaidi huku wakichangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kundi hilo muhimu linapata maeneo rasmi ya kufanyia kazi pamoja na miundombinu bora itakayowawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye tija.
Rais Samia amesisitiza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yanaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi na shughuli za kiuchumi, akitoa mfano wa hali iliyojitokeza wakati wa matukio ya uchaguzi ambapo shughuli mbalimbali za wananchi zilisimama kwa muda.
“Ni wajibu wetu sote Watanzania kulinda amani na mshikamano wa taifa letu. Maendeleo tunayoyataka hayawezi kupatikana bila amani, hivyo kila mmoja wetu ana jukumu la kuilinda,” amesisitiza.
Aidha, amebainisha kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuwataka kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha fursa za ajira na maendeleo.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha maeneo yote yaliyoombwa na Mama na Baba lishe yanatengwa na kuendelezwa kwa ajili ya shughuli zao.
Amesema ni muhimu kwa mamlaka husika kuhakikisha wanapatiwa miundombinu bora, ikiwemo maeneo rasmi ya kufanyia biashara, maji safi, usafi na huduma nyingine muhimu zitakazowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika shughuli za upishi ili kulinda afya za Mama na Baba lishe pamoja na walaji wa huduma zao.
Rais Samia pia ameielekeza Wizara ya Afya kuendelea kutoa elimu ya lishe na usalama wa chakula kwa kundi hilo, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na bora.
Vilevile, ameielekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuimarisha mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mitaji, ili kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo kuendesha shughuli zao kwa tija zaidi.
Ameongeza kuwa Wizara ya Fedha inapaswa kuendelea kuboresha mazingira ya kifedha ili kuwawezesha Mama na Baba lishe kunufaika na huduma za kifedha na kukuza mitaji yao.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa taasisi za utafiti na wadau wengine kushirikiana katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu, akibainisha kuwa matumizi ya nishati hiyo ni muhimu kwa afya na mazingira.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mama Lishe Tanzania (UMALITA), Bi. Julieth Malata amesema Mama na Baba lishe wanamshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kuwawezesha kiuchumi na kijamii, akisema amekuwa chachu ya matumaini kwa wajasiriamali wadogo nchini.
Amesema sera na mipango ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imefungua fursa nyingi kwa wanawake, vijana na makundi maalum, hali inayochangia kukuza uchumi wa wananchi wa kipato cha chini.
Ameongeza kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga ujasiriamali endelevu unaochangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mama na Baba Lishe wanaoshiriki Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe, katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe mfano wa hundi ya Shilingi bilioni 94.158,250,400/= kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Malkia wa Nishati safi kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) Bi. Havijawa Omary katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026
Social Plugin