Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UBORA, NIDHAMU NA UWAJIBIKAJI WAHIMIZWA KWA WATUMISHI WA MAENDELEO YA JAMII KISHAPU

Na Sumai Salum- Kishapu Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Abednego Madole akizungumza kwenye kikao cha Watumishi wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Wilayani humo Aprili 21,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo


Katika hatua ya kuimarisha ujumuishi wa kijamii na kuinua ustawi wa Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeweka msisitizo mkubwa kwenye uibuaji wa vikundi vingi zaidi vya watu wenye ulemavu ili viweze kunufaika na fursa za kiuchumi.


Hayo yamebainishwa Aprili 21, 2026 kwenye kikao cha Watumishi wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii wilayani humo walipokuwa kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo na Mwenyekiti wa kikao hicho akiwa ni Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Abednego Madole, amewataka watumishi kusimamia kwa makini utekelezaji wa majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na nidhamu ya hali ya juu.


Madole amesisitiza kuwa ubora wa kazi sio chaguo ni wajibu hivyo kila mtumishi wa Divisheni hiyo anapaswa kuhakikisha shughuli zote za idara zinatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati, akihimiza utaratibu wa kuhakiki vikundi mara kwa mara pamoja na kuibua vikundi vipya.


"Watumishi wenzangu hakikisheni mnaelekeza nguvu zaidi kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ili visiwe nyuma katika fursa za maendeleo kwa kuwa adhima ya serikali ni kuhakikisha Kila kundi lililokusudiwa linanufaika na mikopo hiyo" amesisitiza Madole.

Afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Juma Ndoera akiwasilisha mada kwenye kikao Cha Watumishi wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii kwa niaba ya Mratibu wa mikopo Aprili 21,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo


Aidha, ameeleza kuwa ni muhimu kuvijengea uwezo vikundi ambavyo bado havijakidhi vigezo ili viweze kushiriki kikamilifu katika mipango ya kiuchumi.


Katika kuhakikisha mikopo inaleta matokeo chanya, Madole amesema utoaji wa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu mikopo hiyo. Akibainisha kuwa elimu hiyo ni chachu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kufikia maendeleo endelevu.


Pia amewataka watumishi kuhakikisha wanatoa elimu endelevu kuhusu ukopaji na urejeshaji wa mikopo kwa wakati ili kujenga nidhamu ya kifedha kwa wanufaika.


Madole amekumbusha kuwa katika utekelezaji wa majukumu na maamuzi yote, watumishi wanapaswa kuzingatia kikamilifu kanuni na miongozo iliyowekwa kwani kufuata taratibu ni nguzo muhimu ya kuhakikisha haki, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.


Katika kikao hicho, washiriki wamepata mafunzo kuhusu ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za mikopo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, matumizi sahihi ya mfumo ikiwemo usajili wa vikundi, mikopo kwa vijana.
Afisa maendeleo ya Vijana Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Athuman Mchekwa akielezea mada inayohusu mikopo mbalimbali yaa vijana


Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya dhati ya Halmashauri ya Kishapu katika kuimarisha utendaji kazi wenye ubora, huku ikiweka mkazo maalum katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kupitia uibuaji wa vikundi imara vitakavyokuwa chachu ya maendeleo jumuishi.


Wajumbe wamekubaliana kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu nidhamu ya mikopo, wakiamini kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za ucheleweshaji wa marejesho na kuongeza mafanikio ya miradi ya vikundi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com