Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KLINIKI YA HIMOFILIA YAZINDULIWA HOSPITALI YA RUFAA MKOA WA SHINYANGA, KURAHISISHA HUDUMA ZA MATIBABU KWA MAGONJWA YA DAMU

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma (wa pili) kulia akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Himofilia na Siko Seli katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Aprili 21,2026 - Picha na Kadama Malunde
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Himofilia na Siko Seli katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Aprili 21,2026
Mratibu wa Mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za magonjwa ya damu na Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania, Dkt. Abdallah Makalla akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Himofilia na Siko Seli katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Augustino Maufi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Himofilia na Siko Seli katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Kliniki ya Himofilia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, hatua inayotarajiwa kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ya magonjwa ya damu na kuimarisha upatikanaji wa huduma hizo karibu zaidi na wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani.

Himofilia ni ugonjwa wa kurithi wa damu unaosababisha mwili kushindwa kugandisha damu kwa kawaida kutokana na upungufu au kasoro katika vinasaba vinavyohusika na kugandisha damu (clotting factors).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Aprili 21,2026 Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Timothy Sosoma amesema tukio hilo ni la kihistoria na lenye umuhimu mkubwa katika juhudi za serikali kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa usawa, bila kujali aina ya ugonjwa au mahali wanapoishi.

Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kupambana na magonjwa ya damu, na kwamba kuanzishwa kwa kliniki hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chama cha Himofilia Tanzania pamoja na wafadhili ikiwemo Novo Nordisk Haemophilia & Haemoglobinopathies Foundation na Novo Nordisk Foundation.
“Tunawashukuru wadau wote waliowezesha kufanikisha upatikanaji wa kliniki hii. Mchango wao umeifanya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kuwa kituo muhimu cha huduma za magonjwa ya damu, hali itakayopunguza mateso kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma,” amesema.

Amesema ugonjwa huo ni wa kurithi na husababisha damu kushindwa kuganda kwa urahisi, hali inayoweza kusababisha mgonjwa kuvuja damu mfululizo.

Ameonya kuwa ugonjwa huo haupaswi kuhusishwa na imani za kishirikina, bali unatakiwa kutibiwa kwa kuzingatia ushauri wa kitabibu.
“Leo tumezindua rasmi Kliniki ya wagonjwa wa himofilia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Ugonjwa huu usihusishwe na imani za kishirikina; mwenye tatizo la kutokwa damu mfululizo afike hospitali kupata matibabu sahihi,” amesema Sosoma.

Ameeleza kuwa kupitia mradi huo, wataalam wa afya wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu namna ya kuwahudumia wagonjwa wa himofilia, yakihusisha kada mbalimbali ikiwemo madaktari, wauguzi, wataalam wa maabara, wafamasia na wataalam wa tiba ya viungo.

Kwa mujibu wa Sosoma, mafunzo hayo hayakuishia katika hospitali ya rufaa pekee, bali pia yamefika katika hospitali zote za wilaya ndani ya mkoa, hatua inayolenga kuhakikisha huduma bora zinapatikana kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu.
“Tumefanikiwa pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa tiba asili, maafisa afya ngazi ya jamii pamoja na wadau wa elimu wakiwemo walimu wakuu na maafisa elimu. Hii inalenga kuongeza uelewa mpana kwa jamii kuhusu ugonjwa wa himofilia na namna ya kuwahudumia wagonjwa,” ameongeza Sosoma.

Aidha, amesema upatikanaji wa dawa za himofilia zinazotolewa bure kupitia Shirika la Himofilia Duniani (WFH) ni mafanikio makubwa kwa taifa, akibainisha kuwa dawa hizo ni ghali sana na ni muhimu katika kuokoa maisha ya wagonjwa na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo.

Katika kusisitiza uendelevu wa huduma, Sosoma ametoa maelekezo mahsusi kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kliniki hiyo inafanya kazi kwa ufanisi akisisitiza umuhimu wa kuteua wataalam maalum watakaosimamia kliniki hiyo, wakiwemo madaktari, wauguzi, wafamasia na wataalam wa fiziotherapia.

Pia ametaka kuwepo kwa mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa dawa ili kuepusha upungufu, akieleza kuwa dawa za himofilia zinazotolewa na wafadhili zina gharama kubwa na zinahitaji usimamizi makini.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa hospitali kuendelea kununua vitendanishi vya maabara ili kuhakikisha vipimo vyote muhimu vinapatikana kwa wakati, pamoja na kuendeleza mafunzo kwa wataalam wengine ambao hawajapata nafasi hiyo.

Katika hatua nyingine, ameagiza kuanzishwa kwa programu za utoaji elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa wa himofilia, akibainisha kuwa elimu ni silaha muhimu katika kupunguza madhara ya ugonjwa huo.

“Ni muhimu sana kuhakikisha tunatunza kumbukumbu sahihi za wagonjwa. Takwimu hizi zitasaidia kupanga huduma, kufuatilia mahitaji ya dawa na kuboresha utoaji wa huduma kwa ujumla,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za magonjwa ya damu na Katibu wa Chama cha Himofilia Tanzania, Dkt. Abdallah Makalla amesema uzinduzi wa kliniki hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kitaifa wa kuboresha huduma za himofilia nchini.

Amesema ugonjwa wa Himofilia ni changamoto kubwa ya kiafya inayohitaji uelewa na huduma maalum, kwani husababisha damu kushindwa kuganda kwa haraka na hivyo kuhatarisha maisha ya mgonjwa.

“Takwimu za kidunia zinaonyesha mtu mmoja kati ya watu 10,000 ana tatizo la Himofilia, na Tanzania inakadiliwa kuwa na watu takribani milioni 67, hivyo inaweza kuwa na wagonjwa 6,700 hadi 13,000 na mpaka sasa wagonjwa waliobainika hapa nchini ni 631 na wanaendelea na matibabu,” amesema Dkt. Makalla.

Makalla ameeleza kuwa mradi huo pia umeiwezesha kwa vitendo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa vifaa na rasilimali muhimu za matibabu.

Amebainisha kuwa hospitali imepokea vitendanishi vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5, vifaa vya mazoezi ya viungo (physiotherapy) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5, pamoja na vifaa vingine muhimu.
“Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na friji maalum kwa ajili ya kuhifadhia dawa za wagonjwa wa Himofilia, friji kwa ajili ya huduma za fiziotherapia, kompyuta kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa, pamoja na vitendea kazi vingine vya zaidi ya shilingi milioni saba,” amesema Dkt. Makalla.

Aidha, ameongeza kuwa mradi huo pia umewezesha upatikanaji wa dawa za Himofilia zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 525 kwa ajili ya kusaidia wagonjwa, hatua inayotarajiwa kuboresha huduma na kupunguza hatari kwa wagonjwa hao.

Hata hivyo, ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa dawa kutoka kwa wafadhili, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuboresha mifumo ya ukusanyaji na utunzaji wa takwimu.
Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Augustino Maufi amesema hospitali hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wagonjwa wa himofilia wanapata huduma bora na za haraka, ili kuepuka vifo na ulemavu unaoweza kusababishwa na ugonjwa huo.

Neema Nicolaus, mkazi wa Shinyanga ambaye ana mtoto mwenye tatizo la himofilia, amesema awali kabla ya kupata elimu kuhusu ugonjwa huo, alimpeleka mtoto wake kwa waganga wa tiba za asili akiamini kuwa ni imani za kishirikina. Amesema hali hiyo ilisababisha mtoto wake kuchelewa kupata matibabu sahihi na hatimaye kupata ulemavu.

Ameongeza kuwa baada ya kupata uelewa sahihi, alimpeleka mtoto wake hospitali ambako ilibainika kuwa ana tatizo la himofilia na siyo kurogwa. Kutokana na hali hiyo, alipatiwa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi, huku akishukuru huduma za tiba ya ugonjwa huo kuanza kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Regina Shirima ameiiomba Serikali ya Tanzania kuwekeza zaidi katika upatikanaji wa dawa za kutibu ugonjwa wa himofilia, akibainisha kuwa gharama zake ni kubwa. Amesema endapo wafadhili wataondoka, wagonjwa wengi watakosa huduma hiyo muhimu na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Mganga wa Tiba Asili, Mabula Joseph, amesema baada ya kupata elimu kuhusu ugonjwa wa himofilia, hawatapokea tena wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo kwa ajili ya matibabu ya asili, bali watawashauri kwenda hospitali ili kupata tiba sahihi na salama.


Himofilia ni nini?

Himofilia ni ugonjwa wa kurithi wa damu unaosababisha mwili kushindwa kugandisha damu kwa kawaida kutokana na upungufu wa vinasaba vya kugandisha damu (clotting factors). Hali hii hupelekea damu kuvuja kwa muda mrefu kuliko kawaida au kutokwa damu ndani ya mwili.

Hata hivyo, takribani asilimia 30 ya wagonjwa hupata himofilia bila kurithi (sporadic hemophilia), hali inayotokana na mabadiliko ya vinasaba (gene mutation) yanayotokea bila historia ya ugonjwa katika familia.

Mtu mwenye himofilia huishi na ugonjwa huu maisha yake yote, kwani hauponi kabisa, lakini unaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi na ya mara kwa mara ili kuzuia madhara makubwa.

Dalili za himofilia ni pamoja na kutokwa na damu ndani ya mwili bila jeraha la wazi, hasa kwenye ubongo, misuli au maungio, pamoja na kuvimba na maumivu kwenye viungo kutokana na damu kuvuja ndani. Vilevile, mgonjwa anaweza kupata kutokwa na damu kwa muda mrefu isivyo kawaida baada ya kupata jeraha, pamoja na kutokwa na damu nyingi baada ya kufanyiwa upasuaji au kung’olewa jino.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com