Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIJANA NA WADAU KAHAMA WAHAMASIKA KUREJESHA OFISI ZA KATA ZILIZOCHOMWA MOTO




Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda akizungumza na vijana wa kahama wakiwemo maofisa usafirishaji wa pikipiki (bodaboda, guta na bajaji) pamoja na mafundi ujenzi mara baada ya kukagua miundo iliyoharibiwa kwa kuchomwa moto ili kufanya tathmini na kuijenga upya

Na Neema Nkumbi, Kahama

Vijana wa Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, wakiwemo maafisa usafirishaji wa pikipiki (bodaboda na bajaji) pamoja na mafundi ujenzi, wamejitokeza kuunga mkono jitihada za serikali katika kukarabati na kujenga upya ofisi za kata na mitaa zilizoharibiwa wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025, hatua inayolenga kurejesha huduma kwa wananchi waliokuwa wakikumbwa na adha ya kukosa huduma za msingi.

Azimio hilo limetolewa Machi 3, 2026 wakati wa ziara maalum iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama kwa kushirikiana na maafisa usafirishaji pamoja na Chama cha Mafundi Ujenzi Kahama (CHAMAUKA), kwa lengo la kukagua athari za uharibifu uliosababishwa na maandamano hayo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema ni muhimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kushirikiana na serikali ili kuhakikisha huduma zinarejea haraka na kuondoa usumbufu unaowakabili wananchi.

“Hatuwezi kuanza kurejesha miundombinu bila kupita na kuona aina na ukubwa wa madhara yaliyotokea, Ni lazima tujue hali halisi kwanza ili tupange namna bora ya kurejesha huduma kwa wananchi,” amesema Nkinda.

Ameongeza kuwa kukosekana kwa ofisi hizo kumesababisha wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kiutawala na wakati mwingine kukosa huduma kwa wakati.

Mwenyekiti wa Chama cha Mafundi Ujenzi Kahama (CHAMAUKA), Baraka Majengo, amesema mafundi wako tayari kutumia ujuzi na nguvu zao kushiriki katika ukarabati na ujenzi wa majengo hayo.

“Sisi kama mafundi tumeona madhara yaliyotokea, tuko tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha ofisi hizi zinajengwa upya na huduma zinarudi kwa wananchi na tutajitolea kwa nguvu zetu,” amesema Majengo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Pikipiki za Biashara Mkoa wa Shinyanga, Idsam Mapande, amesema waendesha bodaboda na bajaji wako tayari kuunga mkono jitihada hizo ikiwemo kusaidia usafirishaji wa vifaa vya ujenzi na mifuko ya saruji pale itakapohitajika.

Wananchi nao wameeleza changamoto wanazokumbana nazo ambapo Asha Maulid, mkazi wa Shunu, amesema wanapata shida kufuata huduma kutokana na ofisi zao kuchomwa moto, huku Edward Ibrahim wa Kata ya Bukondamoyo akisema hali hiyo imeathiri huduma za kijamii katika eneo lao.

Naye Kambai Salum Manyenye, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mhungula, ameziomba mamlaka kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma katika ofisi hizo zinarejea haraka kwa manufaa ya jamii.

Ziara hiyo imekuwa chachu ya mshikamano kati ya serikali na vijana, huku wadau wakiahidi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha miundombinu ya umma inarejeshwa na huduma zinapatikana kama ilivyokuwa awali.

Kata walizotembelea ni Malunga, Mhongolo, Majengo, Nyasubi, Mhungula, Nyahanga na Kahama mjini


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com