SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi imefanikiwa kutoa leseni 129 kwa wazalishaji wa bidhaa katika kanda hiyo, huku leseni 99 kati ya hizo zikitolewa kwa wajasiriamali wadogo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya TBS katika sekta ya viwanda, Meneja wa TBS wa Kanda hiyo, Bw. Hamisi Seleleko amesema hatua hiyo inaonesha jitihada za shirika hilo katika kuwasaidia wazalishaji kufuata viwango vinavyotakiwa na hivyo kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Amesema mafanikio hayo pia yametokana na mahusiano mazuri kati ya TBS na Tawala za Mikoa, Wilaya pamoja na Halmashauri katika kanda hiyo, hali iliyosaidia kuimarisha ukaguzi na utekelezaji wa sheria.
Kutokana na ushirikiano huo, wananchi wamekuwa wakipatiwa elimu ya viwango mara kwa mara jambo ambalo limechangia kupungua kwa bidhaa hafifu sokoni, hususan za chakula na vipodozi.
Bw. Seleleko amesema kiasi cha bidhaa hafifu kilichokamatwa kimepungua kutoka tani 11 mwaka 2024 hadi kufikia tani 8 mwaka 2025.
Aidha, amesema TBS Kanda ya Magharibi imefanikiwa kusajili majengo zaidi ya 2,100 ya chakula na vipodozi, ikilinganishwa na mwaka 2020 wakati ofisi hiyo ilipofunguliwa ambapo majengo 400 pekee ndiyo yaliyokuwa yamesajiliwa.
Amesema hatua hiyo inaonesha kuongezeka kwa uelewa wa wazalishaji na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika uzalishaji wa bidhaa ili kulinda afya na usalama wa watumiaji.



Social Plugin