Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU KAGERA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 57, YAFUATILIA MATUMIZI YA BILIONI 50.2 KATIKA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera Vangsada Mkalimoto

Na Mbuke Shilagi Kagera.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imetangaza mafanikio ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025, ikibainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kudhibiti rushwa, kuimarisha mapato ya Serikali na kusimamia miradi ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 4, 2026 katika ofisi za TAKUKURU zilizopo Manispaa ya Bukoba, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kagera, Bw. Vangsada Mkalimoto, amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo imefanikiwa kusaidia kukusanya jumla ya Shilingi 57,160,177/= zilizotokana na kodi na faini za mizigo ya magari yaliyoingia nchini kwa njia ya magendo kutoka nchini Uganda.

Ameeleza kuwa Desemba 29, 2025, TAKUKURU Wilaya ya Missenyi kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kuzuia Magendo walifanikiwa kukamata magari matano — likiwemo malori matatu na magari mawili ya abiria aina ya Hiace — yaliyovuka mpaka kati ya Tanzania na Uganda pamoja na vituo vya ukaguzi vya Kyaka bila kulipa kodi stahiki. Uchunguzi ulithibitisha kuwa magari hayo yalihusika na uingizaji wa bidhaa nchini bila vibali halali, hatua iliyosababisha Serikali kukusanya mapato husika kupitia kodi na faini.

Katika hatua nyingine, Bw. Mkalimoto amesema TAKUKURU Wilaya ya Muleba imefanikiwa kuokoa matofali 2,830 yenye thamani ya Shilingi 7,924,000/= yaliyokuwa yakitumika katika mradi wa ujenzi wa jengo la OPD katika Kituo cha Afya cha Kata ya Ngenge. Matofali hayo yalibainika kuwa chini ya viwango vya ubora vinavyotakiwa na Serikali, na hatua stahiki zilichukuliwa ili kulinda thamani ya fedha za umma pamoja na kuhakikisha ubora wa miundombinu ya afya.

Aidha, amebainisha kuwa kwa ujumla TAKUKURU Mkoa wa Kagera imefuatilia matumizi ya Shilingi 50,244,425,519.97 katika utekelezaji wa miradi 10 ya maendeleo mkoani humo. Kupitia ufuatiliaji huo, ushauri wa kitaalamu ulitolewa kwa ajili ya kufanya marekebisho katika miradi iliyobainika kuwa na mapungufu, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na kuongeza tija ya matumizi ya fedha za umma.

Mkuu huyo wa TAKUKURU ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa katika maeneo yao, ili kubaini na kuripoti changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na wananchi ni nyenzo muhimu katika kuzuia na kupambana na rushwa, pamoja na kuhakikisha rasilimali za umma zinaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com