Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameitaka jamii kuzingatia haki na usawa kwa wanawake na wanaume ili kujenga jamii yenye maendeleo na mshikamano.
Amesema kuwa usawa wa kijinsia ni msingi muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika elimu, uongozi na shughuli za kiuchumi.
Akizungumza Machi 8, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Wilaya ya Kongwa jijini Dodoma, Senyamule alisisitiza umuhimu wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na mila potofu zinazowanyima wanawake haki zao.
Alieleza kuwa wanawake wakipewa nafasi na kuaminiwa wana uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, aliwahimiza wanawake kuendelea kujitokeza katika shughuli za maendeleo, ujasiriamali na nafasi za uongozi kwa kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa lenye usawa, haki na maendeleo kwa wote.
Mkurugunzi wa Mafunzo na Utafiti Grace Masambaji pamoja na Watumishi wanawake wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ni kati ya watumishi waliohudhuria maadhimisho hayo yaliyoyobeba kauli mbiu ya Haki kwa wanawake na wasichana: Msingi wa Maendeleo jumuishi kufikia Dira 2050.









Social Plugin