Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAFIKI-SDO KUPITIA "MKUA" KUIMARISHA HAKI NA MAENDELEO YA WATOTO KISHAPU


Na Sumai Salum-Kishapu


Shirika la Rafiki-SDO Tanzania limezindua rasmi mradi mpya wa Mpango wa Kuimarisha Azaki (MKUA) katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, kwa lengo la kuwaleta pamoja watoto wa wilaya hiyo ili kujadili changamoto zinazowakabili, ikiwemo elimu, malezi, makuzi na ustawi wao kwa ujumla.


Akizungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Rafiki-SDO Gerald Ng’ong’a, wakati akitambulisha mradi huo Machi, 5,2026, ameeleza kuwa hiyo ni awamu ya pili ya mradi, baada ya awamu ya kwanza kugusa Wilaya tatu za mkoa, Kishapu ikiwa ni mara ya kwanza kwa mradi huu ambapo utagusa Kata zote 29. Lengo ni kuwaleta pamoja watoto ambao ndio walengwa wakuu ili waweze kubaini changamoto wanazopitia na kuunda mbinu za kushughulikia tatizo la watoto kukatisha masomo yao.



Ng'ong'a amefafanua kuwa mradi huu ni mwendelezo wa juhudi zilizolenga kupunguza tatizo la watoto wa mitaani. “Kipindi cha nyuma tulikuwa na ongezeko kubwa la watoto wa mitaani, na baada ya kushirikiana na serikali na mashirika mengine hali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya watoto ambao hawamalizi masomo, na tunataka kubaini sababu na jinsi ya kushughulikia tatizo hilo kikamilifu,” amesisitiza.



"Aidha mradi huu unalenga kuunda mfumo endelevu wa kulinda haki za watoto na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo, jambo ambalo linaweza kuibua mabadiliko chanya katika jamii za mkoa wa Shinyanga kupitia Baraza na Dawati la watoto lakini pia nitumie nafaasi hii kuiomba Halmashauri kutenga bajeti za shughuli za watoto ili tuweze kufanikisha kwa pamoja"Amesema Mkurugenzi Ng’ong’a



Mradi huu unaofadhiliwa na Sida-CANADA kupitia shirika la Save the Children, ukiwa na thamani ya TSH 689,090,027 na kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2026 hadi 2028 ambapo MKUA utasaidia kuimarisha mifumo ya utawala inayolinda haki za watoto na kuunda mazingira yanayowezesha asasi za kiraia kufanya kazi kwa ufanisi.
Mkurugenzi Mkuu Rafiki-SDO, Gerald Ng’ong’a, akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa Mpango wa Kuimarisha Azaki (MKUA) utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Machi,5,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Abednego Madole, amepongeza hatua hiyo na kuahidi kushirikiana kikamilifu.

“Kwanza mmeonesha upendo kwa jamii yetu. Mmeamua kushirikiana na serikali ili kujenga taifa imara lenye nidhamu. Mradi huu utaleta faida nyingi na mabadiliko chanya katika jamii,” amesema Madole.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Abednego Madole akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa Mpango wa Kuimarisha Azaki (MKUA) utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu na shirika la Rafiki-SDO wilayani Hhumo Machi,5,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Shughuli Kuu za Mradi

  • Kuendesha mafunzo na mikutano ya kubadilishana uzoefu na kusaidia uchambuzi unaozingatia usawa wa kijinsia.

  • Kujenga uwezo wa watoto kushiriki katika michakato ya mipango ya bajeti katika ngazi ya Halmashauri za wilaya.

  • Kuendesha usimamizi shirikishi wa kusaidiana katika utekelezaji wa miradi ya kijamii.

  • Kuongeza uelewa na uwezo wa watoto kupitia mabaraza ya wilaya kuhusu mfumo wa ufuatiliaji na utoaji taarifa za haki za watoto chini ya mkataba wa umoja wa Mataifa wa Haki zaMtoto (UNHCRC), ACERWC na CED.Meneja mradi wa Mpango wa Kuimarisha Azaki (MKUA) George Nyamboto akifuatilia kikao cha utambulishaji mradi huo katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Machi, 5,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Utekelezaji wa mradi wa MKUA unatazamwa kama hatua muhimu katika juhudi za kulinda haki za watoto na kuwajengea mazingira bora ya makuzi. Kupitia ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo, jamii ya Kishapu ina matumaini ya kuona watoto wakipata fursa bora za elimu, ulinzi na maendeleo ya kijamii.


Kwa ujumla, ujio wa mradi huu unaimarisha taswira ya Rafiki-SDO kama taasisi inayojali ustawi wa jamii na mustakabali wa kizazi kijacho, huku ukiweka msingi wa ushirikiano imara kati ya wananchi na taasisi mbalimbali katika kujenga jamii yenye usawa, haki na maendeleo endelevu.
Afisa kutoka Rafiki-SDO Magesa Bujashi akifuatilia kikao cha utambulishaji mradi huo katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Machi, 5,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com