.jpg)
Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi ametoa mwito kwa wizara zinazohusiana na sekta ya mazingira zifanye kazi kwa ushirikiano ili kuwa na mpango utakaowezesha uhifadhi endelevu wa mazingira.
Pia, Dk Nchimbi amesihi viongozi wa wizara hizo waongeze jitihada ili Tanzania iwe mfano wa kuigwa katika kulinda na kuhifadhi mazingira, kwa kuwa ina misitu ya kutosha na wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha hilo.
Alisema hayo akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Festo Dugange, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Richard Muyungi pamoja na wataalamu wa wizara hizo Dodoma jana.
Dk Nchimbi alisema wizara hizo zinategemea zaidi uhifadhi wa mazingira, mathalani Wizara ya Maji itafanya kazi kwa ufanisi kama vyanzo vya maji havitaharibiwa, vilevile mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia utawezesha kuokoa ukataji miti ovyo na hivyo kulinda misitu iliyopo.
Alisema Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa kukijanisha nchi na kutoa hamasa za mara kwa mara za upandaji miti, ikiwemo kutumia siku yake ya kuzaliwa kuhamasisha upandaji miti kitaifa, hivyo ni vyema watendaji wote kuongeza bidii kuhakikisha Tanzania inakua kinara wa uhifadhi wa mazingira.
Dk Nchimbi alihimiza viongozi hao kuandaa mpango utakaowezesha kukabiliana na changamoto za kuhifadhi miti baada ya kupandwa ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa na mpango wa upandaji miti kitaifa unaokwenda sambamba na Siku ya Misitu Duniani.
Social Plugin