Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAJULWA: USAWA WA WANAWAKE USIWE KISINGIZIO CHA KUPUUZA WAJIBU WA NDOA NA TENDO LA NDOA


Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, Solomoni Nalinga Najulwa, amewataka wanawake kuhakikisha kuwa madai ya usawa wa kijinsia yanaendana na kutimiza wajibu wao wa asili ndani ya ndoa.

Najulwa ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kilele cha Siku ya Maombi Duniani kwa wanawake wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), tawi la Ndembezi, ambapo alisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya kifamilia kwa pande zote mbili ni njia muhimu ya kupunguza migogoro ya ndoa inayoweza kusababisha vitendo vya ukatili.

Amesema kuwa pamoja na haki wanazozidai, wanawake wanapaswa pia kuzingatia wajibu muhimu ambao haupaswi kupuuzwa, ikiwemo kuwajali waume zao, kuheshimu nafasi ya mwanaume ndani ya familia na kutimiza mahitaji ya msingi ya ndoa, yakiwemo mahitaji ya kihisia na tendo la ndoa.

Najulwa alibainisha kuwa wingi wa majukumu ya wanawake katika shughuli za kiuchumi na kijamii haupaswi kuwa kikwazo cha kutimiza wajibu wao ndani ya ndoa. 

Alisisitiza kuwa kuna mambo ya asili katika mahusiano ya ndoa ambayo hayapaswi kulinganishwa na majukumu ya wanaume, ikiwemo kufanya maamuzi muhimu ya kifamilia bila kuwashirikisha waume zao.

Aidha, alisema kuwa baadhi ya ndoa zimekuwa zikikumbwa na migogoro kutokana na wanawake kuchukua mikopo bila kuwashirikisha waume zao, jambo ambalo wakati mwingine huathiri utulivu wa familia pale wanapolazimika kutumia muda mwingi kuhangaikia marejesho ya mikopo hiyo.

Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia, Najulwa alieleza kuwa kwa sasa vitendo hivyo vinatokea kwa pande zote mbili, wanaume na wanawake, hali inayochangiwa na wanandoa kukosa muda wa kukaa pamoja na kuzungumza ili kutatua changamoto zinazojitokeza ndani ya familia.

Aliongeza kuwa mapambano ya nani mwenye mamlaka zaidi ndani ya ndoa pia yamekuwa chanzo cha migogoro, akiwahimiza wanandoa kujenga utamaduni wa kuheshimiana, kusikilizana na kuzingatia mipaka ya kila mmoja.

Changamoto nyingine zinazochochea ukatili katika ndoa, kwa mujibu wa Najulwa, ni pamoja na kutojali mahitaji na hisia za mwenza, kukosa heshima baina ya wanandoa pamoja na kushindwa kutambua mipaka ya majukumu ya kila mmoja ndani ya familia.

Chanzo _ Radio Faraja

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com