
Na Mwandishi wetu, GEITA
Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi Machi 08, 2026 mkoani Geita na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima utaimarisha fursa za kiuchumi kwa wanawake wa vijijini na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa manusura wa ukatili wa kijinsia (GBV).
Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 104 sawa na Shilingi Bilioni 270.4, umetokana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa kinara wa eneo la Haki na Usawa wa Kiuchumi (Economic Justice and Rights) katika jukwaa la Generation Equality Forum lililofanyika Ufaransa Juni 30, hadi Julai 2, 2021.
Mratibu wa Mradi wa PAMOJA wa OWM-TAMISEMI Bw. Linus Kahendaguza amesema Takribani wanawake 319,850 wajasiriamali wadogo na wakulima wadogo vijijini watanufaika kiuchumi na kuongeza kuwa, wengine 399,000 watanufaika kupitia huduma za kupinga na kukabili ukatili wa kijinsia.
Naye, Mratibu wa Mradi wa PAMOJA wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Adventina Kato amefafanua kuwa, mradi huo ni mkakati jumuishi uliolenga kutekeleza maeneo matatu ambayo ni uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, kinga na mwitikio dhidi ya ukatili wa kijinsia (GBV) pamoja malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (ECD).
Mradi huo wa miaka mitano (5) unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum (WMJJWM) kwa kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, utekelezaji wake ulianza rasmi Aprili 30, 2025 na utamalizika Februari 28, 2029 ambao unatekelezwa katika mikoa 10 ya Arusha, Mwanza, Kagera, Mara, Singida, Shinyanga, Geita, Rukwa,Tabora na Simiyu katika halmashauri 40.
Social Plugin