
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetangaza mpango kabambe wa kuwashirikisha vijana wabunifu nchini katika kuunda mifumo ya Tehama na Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) ili kuleta mapinduzi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hatua hiyo inalenga kupunguza urasimu, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuongeza ufanisi katika mamlaka hiyo inayoshughulika na uchunguzi nyeti wa kisayansi nchini.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, amebainisha hayo jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Dk. Mafumiko ameeleza kuwa katika kipindi kilichopita, mamlaka imefanikiwa kuchunguza sampuli 247,286, zilizosaidia katika kutatua migogoro ya mirathi na utambuzi wa binadamu,kudhibiti mzunguko wa dawa za kulevya nchinina kuhakikisha ubora wa dawa asili, bidhaa za viwandani, na usalama mahali pa kazi dhidi ya kemikali hatarishi.
Hata hivyoi ili kuimarisha uwezo wa uchunguzi, Serikali imewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 32.25 kununua mitambo ya kisasa 32 na vifaa vingine 542 vya maabara. Uwekezaji huu ni fursa kwa vijana wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali, kwani sasa wanaweza kupima ubora wa bidhaa zao kabla ya kuziingiza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Katika hatua inayolenga kukuza wanasayansi chipukizi, GCLA imetangaza punguzo la 75% ya gharama za uchunguzi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya tafiti za kisayansi. Hatua hii inalenga kuondoa kikwazo cha gharama na kuongeza idadi ya tafiti zitakazochochea uvumbuzi nchini.
Usimamizi wa kemikali pekee umechangia kuzalisha ajira 146,567 kupitia usajili wa wadau na utoaji wa vibali vya kuingiza kemikali nchini.
Aidha, mamlaka inaendelea na ujenzi wa ofisi na maabara ya Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam) kwa gharama ya Shilingi bilioni 16.74, huku nyumba za watumishi katika mipaka ya Rusumo, Mutukula, na Namanga zikiwa zimekamilika ili kuimarisha udhibiti wa kemikali mipakani.
Tangazo hili la Mkemia Mkuu kuhusu matumizi ya AI ni ishara kuwa taasisi za Serikali sasa zinaingia kwenye uchumi wa kidijitali kwa vitendo. Hii ni fursa adhimu kwa vijana wa Computer Science na Data Science kushirikiana na wanasayansi wa kemia kutengeneza mifumo itakayorahisisha utambuzi wa sampuli na utatuzi wa kisheria kupitia teknolojia.
Social Plugin