MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefungua ukurasa mpya wa ushindani wa kibiashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kufuatia utekelezaji wa mradi mkakati wa ujenzi wa matangi 15 ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 701.8, unatajwa kuwa mwarobaini wa ucheleweshaji wa meli, hatua itakayookoa mabilioni ya fedha yaliyokuwa yakipotea kama faini za kuchelewa kupakua shehena (demurrage costs).
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbosa, amebainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo Februari 2027, kutashusha muda wa meli kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 22 hadi siku saba pekee.
Mapinduzi makubwa zaidi yanatarajiwa katika gati la kushusha mafuta, ambapo muda wa huduma utapungua kutoka siku saba hadi siku moja. Hatua hii ni pigo kwa gharama za uendeshaji, kwani kila meli inayochelewa ilikuwa ikitoza wastani wa Dola za Marekani 25,000 (takriban Sh milioni 65) kwa siku, gharama ambazo sasa zitafutika na kuleta ahueni ya bei kwa mlaji.
Uwekezaji huu si tu unapunguza gharama, bali unaongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia shehena ya mafuta kutoka tani milioni sita hadi tani milioni 12 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Mbosa, matangi hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 378, yakigusa nyanja zote muhimu za nishati ikiwemo dizeli, petroli, na mafuta ya ndege. Hii inaifanya Tanzania kuwa kitovu cha uhakika wa nishati kwa nchi jirani, ikichochewa na awamu ya pili ya mradi itakayounganisha magati na matangi hayo moja kwa moja kupitia miundombinu ya kisasa ya usafirishaji.
Mikakati hii ni sehemu ya Mpango Kabambe wa TPA (2020-2045) unaolenga kuifanya Tanzania kuhimili ukuaji wa shehena, unaotarajiwa kufikia tani milioni 62 ifikapo mwaka 2030/2031.
Ili kufanikisha azma hiyo, TPA imejipanga kutekeleza miradi ya kipaumbele yenye thamani ya Sh trilioni 12.1, ikiwemo ujenzi wa magati mapya (Namba 12-15), uendelezaji wa Bandari ya Bagamoyo, na ujenzi wa mtandao wa reli ndani ya bandari. Hatua hizi za kijasiri zinathibitisha kuwa Tanzania sasa iko tayari kutumia jiografia yake kutawala uchumi wa bluu na biashara ya kimataifa.
Social Plugin