Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA TAMISEMI YAPITISHA RANDAMA YA BAJETI YA OWM - TAMISEMI NA KUELEKEZA KULETA TABASAMU KWA WANANCHI


Na OWM - TAMISEMI, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imepitisha Randama ya Mpango na Bajeti ya Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2026/27 ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OWM- TAMISEMI)na kuelekeza itakapopitishwa na Bunge utekelezaji wake ukalenge kuwaletea tabasamu Watanzania kwa kuwapatia huduma bora za afya msingi na elimu, ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu bora ya barabara kupitia TARURA.

Maelekezo hayo ya kutaka mpango huo kuwaletea tabasamu Watanzania, yametolewa leo Machi 19, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI, Mhe. Florent Kyombo mara baada ya kamati yake kuipitisha Randama ya Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2026/27.

“Sisi tunatumaini bajeti hii imelenga kuleta tabasamu kwa wananchi kwa kuwapatia huduma bora kama alivyoelekeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza Mhe. Kyombo.

Aidha, Mhe. Kyombo ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI kuipa ushirikiano kamati yake kwa kuipatia taarifa muhimu ambazo zitaiwezesha  kuitetea bajeti hiyo Bungeni, ili ikipitishwa iende kuwa na tija katika kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi, elimu msingi na ujenzi wa miundombinu ya barabara, ikiwa ni pamoja na kuimarisha utawala bora. 
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kuipitisha Randama ya Mpango na Bajeti ya ofisi yake, na kuwahakikishia wajumbe hao kuwa yeye pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI watasimamia kikamilifu utekelezaji wa bajeti hiyo ili kuwaletea Watanzania tabasamu la kudumu.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com