Na Neema Nkumbi, Iringa
Mkoa wa Iringa unaibuka kwa kasi kama kitovu cha rasilimali asilia, utalii na uchumi wa kijani nchini Tanzania, ukiwa mfano halisi wa namna uongozi thabiti na usimamizi bora wa rasilimali unavyoweza kubadili sura ya maendeleo, Kutoka kwenye milima ya Udzungwa hadi uwanda mpana wa Sao Hill, Iringa inabeba simulizi ya matumaini na wajibu kwa taifa.
Katika moyo wa utajiri huo, kunasimama Shamba la Miti la Sao Hill, moja ya mashamba makubwa ya miti barani Afrika, ambalo limekuwa mhimili muhimu wa uzalishaji wa malighafi za viwandani, ajira kwa wananchi na mapato ya serikali, Msitu huu si tu hazina ya miti, bali ni uwekezaji wa muda mrefu unaounganisha uchumi na uhifadhi wa mazingira.
Ziara ya waandishi wa habari iliyofanyika Machi 18, 2026, sambamba na MISA TAN Summit 2026, ilitoa fursa ya kipekee kwa wanahabari kujionea kwa karibu namna rasilimali hizi zinavyosimamiwa na faida zake kwa jamii, Kupitia ziara hiyo, ujumbe uliokuwa wazi ni kwamba Iringa siyo tu kivutio cha utalii, bali pia darasa la usimamizi endelevu wa rasilimali.
Kwa mujibu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 48.1 za misitu, huku takribani hekta milioni 14.5 zikiwa chini ya usimamizi wa wakala huo, Takwimu hizi zinaonesha ukubwa wa sekta ya misitu na nafasi yake katika uchumi wa taifa, huku zikisisitiza umuhimu wa maeneo kama Sao Hill katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya nchi.
Akizungumzia hali halisi ya usimamizi wa msitu huo, Mhifadhi Mkuu wa Sao Hill, Teddy Yoramu, anasema pamoja na mafanikio yaliyopo, changamoto bado zipo hasa moto wa misitu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.
“Watu wengi hudharau madhara ya moto mdogo lakini Ukweli ni kwamba njiti moja ya kiberiti inaweza kuharibu miti iliyochukua hadi miaka 20 kukua ndani ya siku moja,” anasisitiza Yoramu.
Anabainisha kuwa moto huo hauharibu tu miti bali pia huathiri bioanuwai, udongo na vyanzo vya maji, na hivyo kuhatarisha mfumo mzima wa ikolojia na maisha ya binadamu kwa muda mrefu, Hili linaifanya vita dhidi ya moto kwenye misitu kuwa ajenda ya kitaifa inayohitaji ushirikiano wa kila mdau.
Mbali na moto, sekta ya misitu inakabiliwa na shinikizo la matumizi ya ardhi kwa ajili ya kilimo, makazi na shughuli za kiuchumi, pamoja na utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama vyanzo vya nishati, Changamoto hizi zinahitaji mikakati madhubuti ili kuhakikisha rasilimali hizi zinadumu kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wa uongozi wa mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesisitiza kuwa Iringa ina kila sababu ya kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji katika Kanda ya Kusini huku akieeleza kuwa uwepo wa vivutio kama Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Milima ya Udzungwa, pamoja na maeneo ya kihistoria kama Isimila na Kalenga, unaipa mkoa huo nafasi ya kipekee katika ramani ya utalii nchini.
Vivutio hivi vinaongezewa thamani na uwepo wa Sao Hill, ambao mbali na uzalishaji wa miti, unaweza pia kuendelezwa kama kivutio cha utalii wa mazingira (eco-tourism), ukitoa uzoefu wa kipekee kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuitangaza Tanzania kwa kuibua fursa zilizopo na kuhamasisha jamii kushiriki katika utalii wa ndani.
Amesema kupitia uandishi wa habari unaolenga suluhisho, wanahabari wanaweza kubadili mtazamo wa jamii na kusaidia kulinda rasilimali za nchi huku wakichochea ukuaji wa uchumi.
Katika kukabiliana na changamoto zilizopo, serikali imeendelea kuimarisha doria za misitu, kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Hatua hizi zinaendana na Dira ya Taifa ya 2050, inayolenga kuona Tanzania ikiwa kinara barani Afrika katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki lengo ambalo haliwezi kufikiwa bila ushirikiano wa wadau wote.
Kwa mtazamo mpana, mustakabali wa Iringa uko mikononi mwa namna rasilimali zake zinavyotunzwa na kutumika hivyo ni jukumu la serikali, sekta binafsi, wanahabari na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kuwa utajiri huu hauishii kuwa hadithi ya leo pekee, bali urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.
Kwa ujumla, Iringa si tu mkoa wenye rasilimali nyingi, bali ni kielelezo cha Tanzania inayowezekana ambapo utalii, mazingira na uchumi vinaweza kwenda sambamba. Ni mwaliko kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kuja kuona, kujifunza na kuwekeza katika hazina hii adhimu.














Social Plugin